Polisi kuchujwa Kenya

Kenya imeanza mchakato wa kuchuja maafisa wakuu wa polisi 1,600 katika juhudi za kukabiliana na ufisadi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mkuu wa polisi Kenya Mathew Iteere

Mkurugenzi mkuu wa tume ya kupambana na rushwa Patrick Lumumba ameambia BBC kuwa kamati itaangalia kama maafisa hao wamehusishwa na madai ya ufisadi.

Pia wataagiza wakuu hao wa polisi wafanyiwe uchunguzi wa uwezo wao na umakinifu wa kuhudumu katika idara ya polisi.

Mara kwa mara,idara ya polisi ya Kenya imetajwa kuwa idara inayoongoza kwa ulaji rushwa Afrika Mashariki.

Utoaji hongo

Mwaka 2005, mchakato wa kuwaajiri makuruti ilifutiliwa mbali baada ya asilimia 80% ya maombi yaliyowasilishwa kuonekana kuwa walihusika na utoaji hongo au walitumia watu wanaofahamu kupata kazi.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi Anne Waithera anasema shughuli hio ni ya kwanza nchini Kenya na inafanywa kwa nia ya kufanya raia kuwa na imani na idara ya polisi.

Maafisa wote wa cheo cha mrakibu watafanyiwa usaili upya.

"Jambo moja tutakalozingatia ni kama afisa wa polisi anakabiliwa na kesi ambazo zitaingiza dosari maadili yake," Bwana Lumumba ameambia BBC.

Lakini chama kikuu cha wafanyakazi nchini Kenya (Cotu) linataka shughuli hio isimamishwe kwa kuwa wao hakuwakilishwa katika kamati ya mchujo, hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.

"Kama hilo halitafanyika,mchakato huu huenda ukaonekana umefanywa na serikali kuwatimua maafisa wengine ndani ya idara ya polisi," Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi Francis Atwoli alisema.

Kamati imeanza shughuli hio maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Kenya.

Katika mji mkuu Nairobi,shughuli itafanyika wiki ijayo.