Syria kukabiliana na magenge

Waandamanaji wakibeba bendara Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji wakibeba bendara

Serikali ya Syria imeahidi kukabiliana ''vilivyo'' na magenge yaliyojihami yanayolaumiwa kwa vifo vya maafisa wa usalama 120.

Maafisa hao waliuwawa katika mji wa Jisr al-Shughour, ulioko Kaskazini mwa taifa hilo.

Runinga ya kitaifa imesema, mauaji hayo yalitokea Ijumaa iliyopita wakati mamia ya watu waliokuwa wamejihami walichukuwa udhibiti wa mji wa Jisr al-Shughour,ulioko takriban kilomita 20 kutoka eneo la mpaka kati ya Syria na Uturuki, na kutekeleza mauaji hayo .

Waziri wa mambo ya ndani wa Syria nchini humo amesema serikali itatumia nguvu kukabiliana na magenge hayo.

Baadaye, wakazi wa mji huo walionya kuwa huenda kukatokea umwagikaji mkubwa wa damu iwapo maafisa nchini humo watatekeleza tishio lao la kurejesha utulivu kwa nguvu.

Onyo hilo lilitolewa kuptia taarifa iliyotumwa katika mtandao wa upinzani nchini humo.

Wakati huo huo, Ufaransa imesema iko tayari kuuliza baraza la usalama la umoja wa mataifa kupigia kura azimio la kushutumu serikali ya Syria, licha ya kwamba huenda Urusi ikipanga azimio hilo.

Akizungumza mjini Washington, Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Alain Juppe amesema anaamini watapata uungwaji mkono katika baraza hilo la wanachama 15, na pia watajaribu kusihi Urusi kubadilisha msimamo wake.