Wa Syria wamiminika mpaka wa Uturuki

Idadi ya wakimbizi kutoka Syria inaongezeka kwenye mpaka wa Uturuki wakikimbia hofu ya shambulio la serikali kwenye mji wa Jisr al-Shughour ulio kaskazini mwa nchi.

Takriban raia 1,000 wa Syria wamevuka mpaka usiku, kwa mujibu wa afisa wa Uturuki, na kuongezea idadi hiyo kufikia wakimbizi 1600.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption wakimbizi wamiminika Uturuki

Papa Benedict XVI pamoja na Umoja wa Mataifa ameisihi Syria isiwashambulie raia wake.

Ombi hilo linakuja baada ya Uingereza na Ufaransa kupendekeza azimio la Umoja wa Mataifa la kuikashifu Syria kwa kuanyanyasa waandamanaji.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption UN yalaani kunyanyasa raia

Mswaada huo umekaribia kuomba hatua kali zichukuliwe, ingawa bado haifahamiki kama pendekezo litaungwa mkono kiasi cha kupigiwa kura, amesema mwandishi wetu.

Urusi na Uchina zimesimama kidete na kusema zinapinga mswada huo wa azimio, ambapo Urusi imesema Syria iachiwe jukumu la kutatua masuala yake ya ndani bila kuingiliwa na wageni.

Wasiwasi kuwa mji wa Jisr al- Shughour utashambuliwa ni kufuatia madai ya wakuu wa Syria kudai kuwa makundi yenye silaha ndiyo yaliyoua askari 120 wa vikosi vya usalama.

Taarifa hiyo inasema wakuu wa Syria wamesema kuwa ni wananchi wa mji huo waliomba jeshi liingilie kati kurejesha amani.

Hata hivyo habari tofauti zinasema kuwa ghasia hizo zilifanywa na askari wanaoasi jeshi,na kwamba askari watiifu kwa serikali ndiyo waliofanya mauwaji ya raia.

Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa zaidi ya watu 1,000 wameuawa tangu maandamano yaanze mwezi Febuari kupinga utawala dhalimu wa Rais Bashar al Assad na sasa yumkini mamiya ya askari wa vikosi vya serikali wameuawa.

Huku nyuma mswada uliopendekezwa na Uingereza na Ufaransa na kuungwa mkono na Ujerumani na Ureno kuwasilishwa kama azimio linalokashifu ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Syria, unaitaka Syria ikomeshe kwa haraka vitendo vya fujo na kuyapa fursa mashirika ya kibinadamu yaweze kuwafika raia wanaohitaji msaada.

Mswada huo unapendekeza suluhisho kuwa ili mgogoro huo kukomeshwa itabidi kutumia mchakato utakaosimamiwa na wa Syria wenyewe, wazo ambalo wandishi wanasema ni jaribio la kuwashawishi wanachama wa Baraza la usalama wajaribu kujiepusha mfano wa yaliyotokea Libya.