Boko Haram wakiri kulipua polisi Nigeria

Msemaji wa Kundi la Boko Haram ameelezea kuwa kundi hilo lilipanga shambulio hilo kwenye makao makuu ya polisi mjini Abuja.

Taarifa kutoka kundi hilo sasa imethibitisha madai ya polisi kuwa shambulio hilo ambapo watu sita waliuawa limetekelezwa na kundi hilo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Boko Haram inashukiwa huenda wakawa wamehusika katika shambulio

Msemaji wa kundi hilo alipiga simu kwenye ofisi za BBC nchini Nigeria na kukiri kuwa kundi hilo ndilo lililopanga tukio hilo ambalo limezidisha uhasama kati ya kundi hilo na polisi.

Makao makuu ya kundi la Boko Haram ambalo linapinga elimu ya kisasa, yapo Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hata hivyo hivi karibuni, kundi hilo limekuwa likilenga maeneo nje ya kaskazini mwa nchi hio.

Miaka miwili iliyopita vikosi vya usalama viliharibu makaazi ya kundi hilo na kumuua kiongozi wao katika mashambulizi yaliyosababisha mamia ya watu kufa.

Kufuatia shambuli hilo vituo vya polisi katika eneo hilo vimekuwa vikilengwa na washambulizi mara kwa mara.

Katika tukio la alhamisi, bomu lililipuka karibu na makao makuu ya polisi, na kusababisha uharibifu mkubwa wa magari.

Maafisa wa polisi wameelezea kwamba shambulio hilo lilitekelezwa na mtu aliyejilipua.

Shirika la Msalaba Mwekundu limeelezea kwamba kulikuwa na miili mahali hapo, lakini ilikuwa ni vigumu kuhakikisha ni watu wangapi wamekufa.

Shirika hilo linasema watu wasiopungua 6 wameuawa.

Muhammad Jameel Yusha'u wa BBC anasema "Tukio hili limetokea wakati Nigeria inakabiliwa na changamoto kubwa za usalama katika sehemu mbali mbali nchini; lakini zaidi katika siku za hivi karibuni katika maeneo ya kaskazini mashariki kutokana na harakati za madhehebu ya msimamo mkali ya Boko Haram".

Wakati mashambulio ya mabomu katika siku zilizopita yamezusha hofu na wasiwasi kwa wananchi na serikali ya Nigeria, mashambulio katika makao makuu ya polisi ni kama onyo kwa watawala kwamba hali ya usalama si ya kuridhisha, halikadhalika yanabainisha kasoro za usalama katika kitovu cha mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Ni siku chache tu zilizopita mkuu wa polisi Hafizu Ringim alidai kwamba wamejiandaa vilivyo kupambana na madhehebu ya Boko Haram.