Bashir kuondoa majeshi yake Abyei

Rais wa Sudan Omar al-Bashir imearifiwa amejitolea kuondoa majeshi yake kutoka eneo lenye mzozo la Abyei, ambalo limekuwa mwiba katika kipindi hiki Sudan Kusini ikijiandaa kupata uhuru wake mwezi ujao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Moshi ukifuka katika mji wa Abyei

Bw Bashir ameripotiwa kusema hivyo mbele ya kiongozi wa kusini Salva Kiir katika mazungumzo ya Umoja wa Afrika yanayofanyika nchini Ethiopia.

Watu wapatao 140,000 wamekimbia mapigano ya hivi karibuni huko Abyei na mkoa wa karibu wa Kordofan Kusini.

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wamesema makundi yanayounga mkono upande wa kusini yamekuwa yakiandamwa na kuuawa.

Vifo

Sudan kusini inatarajia kujitenga na kaskazini katika mpango wa amani ambao ulimaliza miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kusini na kaskazini, vilivyosababisha vifo vya watu takriban milioni moja na nusu.

Kuna wasiwasi kuwa mapigano ya hivi karibuni huenda yakazusha upya mgogoro huo, ingawa Rais Bashir amesema atakubaliana na uhuru wa kusini.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin amesema taarifa ya nini kitatokea iwapo majeshi ya kaskazini yataondoka bado zinafanyiwa kazi.

Usalama

Bw Bashir na Bw Kiir wanaendelea na mazungumzo yao kwa siku ya pili.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi wanafanya usuluhishi katika mazungumzo hayo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Taarifa ya AU imesema watatilia mkazo suala la kuondoka kwa majeshi kutoka mji wenye mzozo wa Abyei, ambao majeshi ya kaskazini yaliuteka mwezi uliopita.

Mapigano

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mazungumzo hayo pia yatajadili "upelekwaji wa majeshi yanayoongozwa na Afrika ya kulinda usalama, kuhakikisha waliokimbia makazi yao wanarejeshwa haraka, na hatua za mwisho za eneo hilo".

Makundi ya haki za binaadam yameonya kuwa watu wa kusini wanasakwa na majeshi yanayounga mkono upande wa kaskazini yaliyopo katika jimbo la Kordofan. Ingawa jimbo hilo lipo upande wa kaskazini, ni nyumbani kwa jumuiya nyingi zinazounga mkono upande wa kusini na eneo hilo limekuwa likishuhudia mapigano hivi karibuni.