Watatu wafariki 14 wazikwa hai Nairobi

Image caption Shughuli za uokoaji zaendelea

Idadi ya watu waliofariki kufuatia kuporomoka kwa jengo la orofa sita jijini Nairobi sasa imefikia watu watatu.

Watu wengine wapatao 14 wangali wamefunikwa na vifusi vya jengo hilo ambalo lilikuwa linaendelea kujengwa.

Wote watatu waliofariki na hali kadhalika wale ambao wangali wamefunikwa na vifusi walikuwa ni mafundi wa jengo hilo.

Afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la msalaba mwekundu la Kenya, Bi Nelly Muluka, ameimbia BBC kuwa kufikia Jumatano mchana hakuna hata mtu mmoja ambaye ameokolewa toka vifusi jengo hilo.

Michanga ikiporomoka

" Tangu jana shughuli za uokozi haija faulu kumtoa mtu hata mmoja toka vifusi hivyo lakini tungali tunaendelea, hatujakata tamaa", Bi Muluka amesema.

Jengo hilo lililoko mtaa wa Embakasi jijini Nairobi liliporomoka Jumanne saa nne asubuhi, mara tu mafundi kuanza shughuli zao za ujenzi.

Justus Malonza ambae ni mmoja wa mafundi hao lakini alinusurika alisema wakati wa tukio hilo alikuwa chini akijitayarisha kupeleka maji ya ujenzi hadi orofa ya sita. Wakati huo ndio alisikia michanga ikiporomoka toka juu.

" Mara nikasikia udongo umeniangukia na kabla sijajua kilichokuwa kikitendeka nilisika kishindo. Sikujua kilichofuatia. Nimejikuta tu katika gari la kubebea wagonjwa", Malonza alieleza.

Fundi huyo manusura anashukuru kwamba mbali na mshtuko , hakupata majeraha yeyote.

Watu wa kujitolea

Kwa wakati huu bado shughuli za uokozi zinaendelea zikiongozwa na Jeshi la Kenya na polisi wakishirikiana na shirika la Msalaba Mwekundu, maafisa wa baraza la mji wa Nairobi, kikosi cha zima moto na watu wa kujitolea.

Image caption Dkt James Kisia

Naibu katibu Mkuu wa shirika la Msalaba mwekundu la Kenya Daktari James Kisia amesema kadiri muda unavyokwenda ndivyo uwezekano wa kuwakuta waliokwama kwenye vifusi hivyo wakiwa hai unavyozidi kididimia.

" Jana tulikuwa tunaweza kuwasiliana na wale ambao wamekwama lakini leo hali ni tufauti, hatuwasikii kabisa.Pengine wanajaribu kuhifadhi nguvu na pumzi zao kwani hawajakula kitu chochote tangu walipokwama", Dkt Kisia ameeleza.

Hii sio mara ya kwanza kwa kisa kama hiki kutokea nchini Kenya.

Ufisadi

Mwaka 2006, jengo moja liliporomoka mjini Nairobi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10 na kuwajeruhi wengine 70.

Miaka mitatu baadaye jengo lengine ambalo lilikuwa lingali linajengwa liliporomoka wilayani Kiambu karibu na Nairobi na kusababisha vifo vya watu sita.

Mbunge wa Embakasi Ferdinand Waititu , analaumu maafisa wa serikali na wa mabaraza ya miji kwa ongezeko la matukio ya majumba kuporomoka.

Mbunge huyo anasema licha ya kwamba mabaraza ya miji yana wahandisi wengi waliohitimu lakini ugonjwa mkubwa ni ufisadi kwani maafisa hao wanaidhinisha ujenzi kinyume na sheria na pia kutofuatilia ili kuangalia jinsi ujenzi unavyoendelea.