Obama atetea hatua ya kutuma jeshi Libya

Rais Barack Obama hahitaji idhini ya bunge la congress kuwatuma wanajeshi wa Marekani kuhusika katika operesheni za Nato nchini Libya.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption White House inasema wanajeshi wa Marekani wanahusika katika majukumu madogo sana nchini Libya

Kulingana na maelezo ya ikulu ya White House, Rais Obama ana uhuru kutuma wanajeshi hao kama kiongozi wa taifa.

Lakini kulingana na sheria iliotungwa wakati wa vita vya Vietnam, rais wa Marekani lazima apate idhini ya bunge la congress kutuma wanajeshi kuhudumu katika nchi ya kigeni ikiwa muda huo utachukua zaidi siku sitini.

Wabunge nchini Marekani wanasema Rais Obama amekiuka sheria hio kwa kuwa muda wa siku sitini ulikwisha mwezi May 20.

Lakini White House imewasilisha taarifa katika bunge hilo, ikielezea kuwa jukumu la wanajeshi wa Marekani ni la kusaidia tu kikosi cha Nato.

White House imesema majukumu ya jeshi la Marekani nchini Libya sasa hivi hayajafikia kiwango ambacho kimewekwa kwenye sheria hiyo ya mwaka wa 1973 ambapo rais atalazimika kuomba idhini ya congress.

Wanjeshi wa Marekani wanasaidia kuongeza ndege za Nato mafuta na katika shughuli za kijasusi nchini Libya, kulingana na maelezo ya White House.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani hawapo kwenye makabiliano na jeshi la Libya, kwa hivyo hawako vitani.

Kulingana na katiba ya Marekani, bunge la congress ndio lenye uwezo wa kutangaza vita.

Ifikiapo jumapili wiki hii, Marekani itakuwa imehusika kwenye harakati hizo za Nato nchini Libya kwa jumla ya siku tisini.