Mafundi 14 wazikwa kwenye vifusi Nairobi

Baada ya siku tatu ya kujaribu kuwaokoa watu wapatao 14 waliofunikwa na vifusi vya jumba la orofa sita lililoporomoka jijini Nairobi,shughuli za uokoaji zakatizwa.

Image caption Maua kuwaaga waliochwa kwenye vifusi

Kufikia wakati wa waokoaji kuondoa mashine na vifaa vyao katika eneo la mkasa, ni miili minne peke yake ndio ilikuwa imepatikana na tayari imekabidhiwa jamaa zao.

Maiti hizo ni za wanaume watatu na mwanamke mmoja ambao walikuwa ni wajenzi katika jengo hilo, eneo la Embakasi.

Sherehe ndogo ilifanywa ya kukamilisha shughuli ya uokozi na kisha maua yakawekwa mahali hapo kwa heshima ya waliofariki.

Maafisa wa Msalaba mwekundu nchini Kenya wanasema shughuli hizo ambazo zilikuwa zikiongozwa na jeshi la Kenya zilifikia kikomo pale waokoaji walipofika hadi sehemu mmoja ya orofa ya chini kabisa na kukukosa watu au miili zaidi.

Msalaba mwekundu

Bi Nelly Muluka ,ambaye ni afisa wa mawasiliano wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya anasema hukukuwa na uwezekano wa kupata watu au hata maiti zaidi.

" sijui kama bado wako chini ya vifusi au la; lakini tulifanya kazi tulivyoweza na tulipofika mwisho tuliweza tu kupata miili ya watu wanne , ", Bi Muluka aeleza.

Lakini Waokoaji wa kujitolea, wakiwemo wanakijiji, waliteta wakidai kuwa kwenye vifusi hivyo bado kulikuwa na maiti zaidi, wengi wakiwa ni ndugu na marafiki.

Jengo hilo lililoko mtaa wa Embakasi jijini Nairobi liliporomoka Jumanne saa nne asubuhi, mara tu mafundi kuanza shughuli zao za ujenzi.

Justus Malonza ambae ni mmoja wa mafundi hao lakini alinusurika alisema wakati wa tukio hilo alikuwa chini akijitayarisha kupeleka maji ya ujenzi hadi orofa ya sita. Wakati huo ndio alisikia michanga ikiporomoka toka juu.

Image caption Siku ya kwanza ya uokoaji

" Mara nikasikia udongo umeniangukia na kabla sijajua kilichokuwa kikitendeka nilisika kishindo. Sikujua kilichofuatia. Nimejikuta tu katika gari la kubebea wagonjwa", Malonza alieleza.

Fundi huyo manusura anashukuru kwamba mbali na mshtuko , hakupata majeraha yeyote.

Sio mara ya kwanza.

Hii sio mara ya kwanza kwa kisa kama hiki kutokea nchini Kenya.

Mwaka 2006, jengo moja liliporomoka mjini Nairobi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10 na kuwajeruhi wengine 70.

Miaka mitatu baadaye jengo lengine ambalo lilikuwa lingali linajengwa liliporomoka wilayani Kiambu karibu na Nairobi na kusababisha vifo vya watu sita.

Wakati huo shughuli za uokoaji zilikatizwa baada ya zoezi la siku nne na kuacha maiti wapatao 16 chini ya vifusi vya jengo hilo la Kiambu.

Sasa pia wakaazi wa Nairobi wanahofia kwamba watu wapatao 14 huenda wameachwa chini ya vifusi vya jengo hilo.