NATO yakiri ilifanya makosa

Image caption hasara ya mabomu mjini Tripoli

NATO imekubali kuwa "matatizo ya mtambo wa silaha" huenda yalisababisha mashambulio dhidi ya raia Jumapili asubuhi mjini Tripoli,Libya.

Katika taarifa,muungano huo wa majeshi umesema kuwa lengo ilikuwa ni kituo cha makombora cha kijeshi,lakini "inaonekana moja ya silaha"haikulenga kituo hicho.

Awali serikali ya Libya ilisema kuwa Nato imeshambulia eneo la makaazi ya watu,na kuwaua raia tisa,wakiwemo watoto.

Nato inatekeleza makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuwalinda raid wa Libya kutoka kwa vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi.

'Familia ilishambuliwa'

"Nato inajutia kufarikia dunia kwa raia na inachukua hatua za makini katika kushambulia utawala ambao unatumia nguvu dhidi ya raia wake wenyewe," alisema Luteni Jenerali Charles Bouchard, kamanda wa harakati hizo.

" Ingawa bado tunachunguza sababu za tukio hili,ishara zinaonyesha kuwa ni matatizo ya mtambo wa silaha huenda yakawa sababu ya tukio lenyewe,"aliongeza.

Taarifa hio ilisema kuwa mashambulio zaidi ya 11,500 yamefanywa na "kila shambulio linapangwa na kutekelezwa kwa makini ili kuepuka mauaji ya raia".