Tunisia:Ben Ali akanusha madai yote

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ben Ali amekanusha mashitaka

Rais wa Tunisia aliyeondolewa madarakani Zine al-Abidine Ben Ali amekanusha madai yote dhidi yake siku moja kabla ya kuanza kwa kesi yake bila ya yeye mwenyewe kuwepo mahakamani.

Bwana Ben Ali alikimbilia nchini Saudi Arabia tarehe 14 Januari kufwatia mapinduzi ya kiraia nchini mwake.

Mawakili wake wanasema hii ni njama ya serikali ya mpito ya Tunisia kubadilisha mawazo ya watu baada ya wao kushindwa kurudisha hali ya amani nchini.

Anaweza kufungwa jela hadi miaka 20 iwapo atapatikana na hatia ya makosa mbali mbali,ikiwa ni pamoja na ufisadi na ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Lakini serikali ya Saudi bado haijaitikia wito wa Tunisia wa kutaka kuwarudisha kwao Bwana Ben Ali na mkewe, Leila Trabelsi, na uwezekano wa wao kufika mahakamani binafsi ni mdogo mno.

'Haki kwa mshindi' Serikali ya Tunisia imeandaa kesi kadhaa dhidi ya Bwana Ben Ali,lakini kesi ya Jumatatu itaangazia zaidi masuala yanayohusiana na pesa,silaha na madawa ya kulevya zinazodaiwa kuachwa kwenye kasri zake.

Bwana Ben Ali pia anachunguzwa kwa kushukiwa kutekeleza mauaji,matumizi mabaya ya madaraka, kusafirisha kinyume cha sheria vitu vya jadi na biashara haramu ya pesa.