Uchina yatetea ziara ya Rais Bashir

Maafisa wa serikali ya Uchina wameutetea uwamuzi wa serikali yao wa kumualika Rais Omar al Bashir wa Sudan wiki ijayo, hatua hii inafuatia shutuma kutoka makundi ya kutetea haki za binadamu.

Haki miliki ya picha afp
Image caption Rais wa Sudan

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni Hong Lei amesema serikali yake ina kila haki ya kumualika Rais Bashir.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC ilitoa agizo la kumkamata Rais Bashir kwa tuhuma za mauwaji ya kimbari na uhalifu wa kivita mwaka 2009.

Lakini Bw. Hong amesema Uchina haijatia saini mkataba wa mahakama hiyo ya kimataifa ya ICC.

Tangu ICC ilipotoa hati ya kumkamata, Rais Bashir amezuru nchi za Eritrea, Misri, Libya na Qatar, nchi zote hizo hazijatia saini mkataba wa kuitambua ICC.

Hong ameongeza kuwa Rais Bashir aliizuru Kenya ambayo iliamua kutomkamata licha ya kuwa Kenya imetia saini mkataba wa ICC, mkataba ambao unawawajibisha wote waliotia saini kumkamata yeyote anayetakiwa na mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International wiki iliyopita liliihimiza Uchina imkamate kiongozi huyo wa Sudan.

Catherine Baber afisa kutoka shirika hilo amesema Uchina itakuwa maficho ama ngome ya wanaodaiwa kuhusika na mauwaji ya kimbari.

Mahakama hiyo imemshtaki Rais Bashir kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na mauwaji ya kimbari katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Uchina imewekeza raslimali nyingi nchini Sudan na imekuwa katika mstari wa mbele kuiunga mkono serikali ya Bashir.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii