Wabunge walazimishwa kulipa kodi Kenya

Mamlaka ya ushuru nchini Kenya (KRA) imeagiza kuwa wabunge wote walipe kodi kulingana na katiba mpya nchini humo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wabunge wanasema hawawezi kulipa kiasi hicho cha pesa

Mamlaka hiyo imewataka wabunge hao walipe malimbikizi ya kodi hiyo kutoka mwezi Agosti mwaka jana, wakati katiba mpya nchini humo ilipoidhinishwa.

Kulingana na makadirio ya KRA, kila mbunge anatakiwa kila dola 10,000 kutoka mshahara wake.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa wabunge nchini Kenya wapo kwenye orodha wa wawakilishi wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi barani Afrika.

Agizo hilo la mamlaka ya ushuru hata hivyo limepingwa vikali na baadhi ya wabunge wanaosema kuwa huenda wakashindwa kumudu maisha kufuatia hatua hiyo wasiokuwa wakiitarajia.

Akizungumza na BBC, Waziri wa Maji ambaye pia ni mbunge wa eneo la Kitui, Bi Charity Ngilu amesema kuwa kulipa pesa hizo itakuwa kibarua kigumu sana.

"Tulipoingia bunge tulielezewa pesa ambazo tutalipwa katika kipindi cha miaka mitano kisha wengi wakachukua mikopo, sasa kuja sasa hivi na kutuambia tulipe, itakuwa vigumu sana kwa kuwa hatuna biashara" alisema Bi Ngilu.

Wabunge wengi walitegemea kuwa agizo hilo kuwa walipe kodi litaanza kutekelezwa baada ya uchaguzi ujao mwakani.

Kwa sasa wanamakubaliano na Rais Kibaki kuwa wasilipe kodi hiyo lakini hakuna muafaka ikiwa hali itakuwa hivyo.

Mwaka jana wabunge waliongeza mishahara yao hadi dola 126,000.

Uamuzi huo ulikemewa vikali na raia nchini humo ambao wengi wanakipato cha chini ya dola moja kwa siku.