Serikali ya Ugiriki yaponea kura ya kuwa na imani

Raia wa Ugiriki wakiandamana
Image caption Raia wa Ugiriki wakiandamana dhidi ya serikali ya nchi hiyo

Serikali ya Ugiriki imeshinda kura ya kuwa na imani nayo bungeni wakati ambapo inapofanya bidii kutafuta kuungwa mkono katika mipango yake ya kufufua uchumi wa nchi hio.

Baraza jipya la Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou liliungwa mkono kwa jumla ya kura 155 huku 143 wakilipinga na wabunge wawili wakikataa kupiga kura.

Sasa wabunge wataombwa kupitisha mapendekezo ya kubana matumizi kwa Pauni billioni 25, kuokongeza ushuru, mageuzi ya kifedha na mipango ya ubinafsishaji.

Mawaziri wa muungano wa Ulaya wanasema ni lazima bunge la Ugiriki lipitishe mapendekezo hayo ili nchi iweze kupokea msaada wa euro bilioni 12 kulipia madeni yake.

Mapema maelfu ya watu walikusanyika nje ya majengo ya bunge kupinga mapendekezo hayo na wanasiasa kwa ujumla. Walipaaza sauti zao: " Wezi ! Wezi!"

" Naamini afadhali tufilisike na tusahau mara moja " . Mikakati hii inatuua taratibu," Efi Koloverou, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 aliliambia shirika la habari la Reuters. " Tunataka watu wenye ujuzi, wanaojua kazi zao kuchukuwa hizi nafasi".

Bwana Papandreou alilifanyia baraza lake la mawaziri mageuzi na kufuatia misururu ya maandamano kuhusu swala la uchumi linavyoshughulikiwa,akambadilisha waziri wake wa Fedha.

Kura hio ya kutaka kuungwa mkono ilifanyika siku ya Jumatano. Hii ni baada ya mjadala mkali siku ya Jumanne, baadhi ya wabunge wa upinzani walitoka bungeni kwa muda.

Mapema Waziri Mkuu alikiri kuwa hatua hizo za kufufua uchumi ni kali mno lakini jambo ambalo Ugiriki haliko tayari kufanya kwa wakati huu ni kufanya uchaguzi.