Waliokuwa waasi Congo 'wabaka wengi'

Wafanyakazi wanaotoa misaada wanafanya uchunguzi wa ripoti iliyosema takriban wanawake 60 wamebakwa karibu na mji wa Fizi uliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ubakaji huo wa wanawake wengi unadaiwa kufanywa na kundi la waliokuwa waasi ambao hivi karibuni waliasi jeshi la serikali, ambao waliungana chini ya makubaliano ya amani.

Majeshi kutoka kundi hilo hilo hivi karibuni walishtakiwa kwa kubaka takriban wanawake 50 huko Fizi siku ya mwaka mpya.

Image caption Wanawake wakiandamana Congo kupinga ubakaji

Ujumbe wa umoja wa mataifa mwaka jana uliipa jina nchi hiyo ya DRC "mji mkuu wa ubakaji duniani".

Miaka 16 ya ghasia mashariki mwa Congo imejulikana kwa udhalilishaji wa wanawake na wasichana.

Zaidi ya wanawake 300, wanaume na watoto walibakwa na muungano wa kundi la waasi kwenye mji wa Luvungi na vijiji jirani katika jimbo la Kivu Kaskazini ambalo halikuwa mbali sana na kituo cha umoja wa mataifa mwezi Agosti 2010.

Tukio la hivi karibuni lilitokea vijijini karibu na Fizi, Kivu kaskazini kati ya Juni 10 na 12 lakini ndio kwanza imeripotiwa.

Jean-Marie Ngoma, mwanachama wa bunge la jimbo hilo, ameiambia redio inayofadhiliwa na umoja wa mataifa ya Okapi kuwa zaidi ya wanawake 60 walibakwa kwenye kijiji cha Nyakiele peke yake.