Tsvangirai ni tisho kwa usalama

Afisa mmoja wa ngazi za juu katika jeshi la Zimbabwe amemshutumu Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai akisema kuwa yeye ni tisho kwa usalama.

Image caption Morgan Tsvangirai Waziri Mkuu wa Zimbabwe

Brigadia Jenerali Douglas Nyikayaramba amesema haya katika gazeti la taifa la Herald.Ameongeza kuwa Tsvangirai anafuata maagizo ya wageni wanaotaka kuleta mageuzi haramu ya utawala.

Matamshi haya yametolewa wakati Tsvangirai amewataka wakuu wa jeshi wavue sari zao za jeshi ikiwa wanataka kushindana nae kisiasa katika uchaguzi ujao.

Bw Tsvangirai alijiunga katika serikali ya umoja wa kitaifa na Rais Robert Mugabe mwaka 2009.

Mseto huo uliochukuwa hatamu za uwongozi baada ya uchaguzi uliogubikwa na mvutano mwaka 2008, umesaidia kuufanya uchumi kuwa thabiti kwa kiasi na vile vile kupunguza ghasia za kisiasa nchini humo.

Lakini utawala huu umekumbwa na mizozo ya ndani kwa ndani kuhusu mpango wa kuleta mabadiliko.

Rais Mugabe na chama chake cha Zanu-PF amekuwa akitaka uchaguzi ufanywe mwaka huu lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa na wasiwasi kutokana na taarifa zinazosema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya kuwanyanyasa wapinzani wake.

Chama cha Waziri Mkuu cha MDC kinavitaka vikosi vya usalama vijiepushe na masuala ya siasa na kutoonesha hadharani kumuunga mkono Rais Mugabe katika uchaguzi ujao.

Wengi kati ya wakuu wa vikozi vya usalama nchini Zimbabwe pamoja na Rais Mugabe walipigana wakati wa vita vya miaka ya 70 dhidi ya utawala wa wazungu waliokuwa chache, wakuu hawa bado wamedumisha uhusiano wa karibu na Rais Mugabe.

Katika uchaguzi wa mwaka 2008 jeshi lilishutumiwa kuwa lilihusika katika mashambulizi yaliofanywa dhidi ya wafuasi wa Morgan Tsvangirai.

Brigadia Jenerali Douglas Nyikayaramba aliongeza kusema kuwa Rais Mugabe ataondoka mamlakani tu wakati atakapotaka yeye ama akifa na kwamba yeye mwenyewe amejitolea maisha yake kuhakikisha kuwa Rais Mugabe anasalia madarakani.

Chama cha MDC kinasema bila ya kuwepo na katiba mpya na mabadiliko katika utaratibu wa uchaguzi, basi uchaguzi ujao hutokuwa huru na wa haki.

Rais Mugabe na wenzake wanasema matatizo ya kiuchumi yanayoikumba Zimbabwe yametokana na njama zinazopikwa dhidi yake kumng'atua mamlakani kutokana na sera yake ya kuyachukuwa mashamba yaliokuwa yanamilikiwa na wazungu.

Wanaompinga wanasema ameibadili Zimbabwe kutoka nchi iliyotambulika kuwa na uchumi imara zaidi barani Afrika hadi nchi ambayo uchumi wake umeporomoka.