Song apigwa faini

Mchezaji wa kiungo cha kati wa Arsenal, Alex Song, amepigwa faini na shirikisho la mchezo wa soka nchini Cameroon, kufuatia mzozo uliozuka kati yake na mshambulizi Samuel Eto'o.

Image caption Mchezaji wa Cameroon Alex_song

Eto'o hakupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na kamati kuu ya nidhamu ya shirikisho hilo Fecafoot.

Mchezaji wa Tottenham Hotspurs, Benoit Assou-Ekotto naye alipewa onyo na kamati hiyo ya nidhamu.

Mashtaka dhidi ya wachezaji hao yalihusiana na mchuano wa kufuzu kwa kombe la taifa bingwa barani Afrika dhidi ya Senegal tarehe 4 mwezi Juni na pia katika kambi ya mazoezi kabla ya mechi hiyo.

Song alikataa kumsalimia Eto'o wakati wawili hao walipokutana kabla ya mechi hiyo.

Wawili hao walikuwa wametofautiana wakati fainali za kombe la dunia nchini Afrika Kusini na mechi hiyo ilikuwa mechi ya kwanza ya Song tangu fainali hizo na timu hiyo ya taifa.

Song alipigwa faini ya US$2,000 na pia kuamriwa kufanya mazoezi ya siku tatu ya timu ya taifa ya vijana chipukizi mwaka ujao.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Samuel Eto'o

Eto'o alikabiliwa na mashtaka ya kukosa kufika kambini na pia kumdharau kocha wa timu hiyo Javier Clemente wakati mchezaji huyo alipopinga mabadiliko yaliyotekelezwa na kocha huyo.

Hata hivyo mashtaka hayo dhidi ya Eto'o yalifutiliwa mbali, baada ya uchunguzi kufanyika.

Assou-Ekotto, ambaye hakufika katika kikao cha kamati hiyo, amepewa onyo pia kwa kukosa kuitikia wito wa kufika kambini.

Timu ya Indomitable Lions inakabarua kigumu kufuzu kwa fainali za kombe la taifa bingwa barani Afrika zitakazoandaliwa nchini Equatorial Guinea na Gabon mwaka ujao.

Timu hiyo inashikilia nafasi ya tatu kundi lao alama 5 nyuma na Senegal na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.