Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Pweza kuchuana

Pweza wanane nchini Ujerumani watashindanishwa kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia la soka kwa wanawake itakayoanza hivi karibuni.

Pweza hao watashindanishwa kutafuta mrithi wa pweza Paul, aliyepata umaarufu wa kutabiri matokeo ya mechi za soka za Kombe la Dunia mwaka jana Afrika Kusini.

"Kwa sasa tunawafanyia mazoezi na mafunzo tukiwa na matumaini ya kupata japo mmoja atakayeweza kutabiri" amesema Britta Analauf, msemaji wa idara inayoandaa michuano ya Kombe la Dunia.

Kila siku kuanzia saa tano kamili asubuhi pweza hao wanane, waliopo katika miji tofauti watakuwa wakipewa mitihani ya kutabiri mambo mbalimbali.

Pweza hao wanatoka miji ya Hanover, Koenigswinter, Konstanz, Minich, Speyer, Timmendorfer Stand, na mji aliotoka Paul, Oberhausen.

Utabiri huo wa mazoezi haujatajwa rasmi, lakini gazeti la Metro limesema itakuwa ikilingana kidogo na kile alichokuwa akifanya Pweza paul mwaka jana, pale alipojizolea sifa za kubashiri sawasawa matokeo ya mechi zote saba za Ujerumani.

Pweza Paul alifariki dunia akiwa na umri wa karibu miaka mitatu, mwezi Oktoba mwaka jana.

Jela afadhali

Bwana mmoja nchini Marekani anatarajiwa kwenda jela, baada ya kuingia benki na kutaka kuiba dola moja.

Gazeti la Telegraph limesema Bwana huyo James Richard Verone, aliingia benki na kumwambia mfanyakazi wa benki kuwa amekuja kuiba, na anataka dola moja tu.

Baada ya kutoa madai yake hayo, bwana huyo mwenye umri wa miaka hamsini na tisa, aliketi chini, na kusubiri polisi waje kumkamata.

Mwizi huyo, ambaye hana kazi na anakabiliwa na maradhi, amesema lifanya uhalifu huo, ili akamatwe na kufungwa, kwa kuwa anaamini jela ndio mahala pekee atapata huduma za afya.

"Mimi ni mtu wa busara" amesema bwana James "Nilitaka kuweka wazi kuwa nia yangu sio kuiba pesa, bali nahitaji kupelekwa hospitali".

Bwana huyo, ambaye hakutumia silaha yoyote wakati akifanya wizi hu, amesema ana imani kuwa huenda akapewa hukumu ya kifungo cha miaka mitatu jela, huku akipata huduma za hospitali.

Wizi huo ulitokea katika benki ya RBC, North Carolina.

Maisha ni mafupi

Haki miliki ya picha BBC World Service

Mwanamama mmoja nchini Urusi alikufa kutokana na mshituko wa moyo, baada ya kuamka na kukuta watu wakiwa katika mazishi yake, wakidhani alikwisha kufa.

Mwanamama huyo, mwenye umri wa miaka arobaini na tisa, alitajwa na madaktari kuwa ubongo wake haufanyi kazi, na hivyo madaktari kusema tayari amekufa. H

ata hivyo, hakuwa amekufa, lakini alikufa kikweli kweli, baada ya kusikia watu wakiomboleza na kumfanyia sala kuomba roho yake ilale salama.

Wakati waombolezaji wakipita mbele ya jeneza, walishitushwa, baada ya mwanamama huyo waliyedhani amekufa, kuamka ghafla na kuanza kupiga kelele.

Gazeti la The Express limeripoti kuwa, saa arobaini na nane kabla ya hapo, mume wa mwanamama huyo alikuwa ameambiwa mke wake amekufa.

Baada ya kuzinduka, bila kutarajiwa, na hatumaye kufa, mume wa mama huyo Fagili Mukhametzyanov alisema "Yaani alikuwa akipepesa macho, na mara moja tukampeleka hospitali.

Hata hivyo alikaa kwa dakika kumi na mbili tu, na kufariki, na safari hii, alikufa kikweli, amesema mume huyo.

"Nimekasirishwa sana, nataka kujua kilichotokea," amesema mtu huyo. "Hakuwa amekufa wakati waliponiambia, angeweza kupona" ameongeza mume huyo kwa hasira, akizungumza na gazeti la Austrian Times.

Msemaji wa hospitali alipotibiwa mama huyo, amesema wanalifanyia uchunguzi suala hilo.

Mkeketo kweli

Haki miliki ya picha webmd

Bwana mmoja nchini Sweden ambaye alikuwa akilalamika maumivu ya tumbo kwa miaka ishirini na tano,

amekutwa na kijiko cha mbao tumboni mwake. Madaktari wanahisi huenda kijiko hicho chenye ncha kali, kilisahaulika tumboni mwa mtu huyo wakati alipofayiwa uspasuaji wa tumbo miaka 25 iliyopita.

Shirika la habari la Sweden, TT, limeripoti siku ya Alhamisi kuwa bwana huyo, Ove Sohlberg mwenye umri wa miaka sitini na mitano alikuwa akisumbuliwa sana na maumivu ya tumbo.

"Nimelazwa hospitali zaidi ya mara mia moja katika kipindi hicho kutokana na maumivu" amesema bwana Sohlberg.

"Nilikuwa nahisi kama kuna kitu ndani, maumivu yalikuwa hayaishi" amesema bwana huyo.

Wiki iliyopita, kundi la madaktari hatimaye walifanikiwa kutoa kipande cha mbao, chenye ncha kali kama toothpick, kutoka ndani ya tumbo la bwana Sohlberg.

Bwana huyo amesema amefurahi kuondoa kijiko hicho ambacho kimekaa tumboni mwaka kwa robo karne. "Inasikitisha kidogo, kwa kuwa nililazimika kuishi hivyo kwa miaka mingi, nikiumwa na tumbo" amesema.

Sufuria la dhahabu

Haki miliki ya picha flickr

Sufuria la kupikia la bei ghali zaidi duniani linauzwa.

Sufuria hilo linauzwa yuan za Uchina milioni tatu nukta nane, sawa na karibu dola laki nane za kimarekani.

Sufuria hilo lina vishikio vya dhahabu, na mfuniko wake pia una kishikio cha dhahabu halisi, na uzito wake ni gramu mia saba na thelathini na nane, huku pia likiwa na vipande kumi na tatu vidogo dogo vya almasi.

Kwa mujibu wa gazeti la Metro, sufuria hilo linauzwa katika duka moja huko Changchun, katika makao makuu ya jimbo la Jilin nchini Uchina.

Na iwapo utataka kulinunua, na ukisha weka order yako, sufuria hilo litaletwa kwako na gari la kifahari la Rolls Royce, ingawa hutopewa hilo gari.

Na mteja atakayeagiza sufuria hilo, atapewa mualiko wa yeye pamoja na marafiki zake kumi kwenda katika hoteli moja ya kifahari nchini Ujerumani, kwenda kukabidhiwa bidhaa aliyoagiza.

Msemaji wa duka hilo, Fissler, amesema mteja wa sufuria hili atapatiwa huduma ya hali ya juu kabisa.

Sufuria ya bei ghali...ujue na kupika basi...

Na kwa taarifa yako.... Pweza ana mioyo mitatu

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa