Simba yaunguruma Kagame

Simba
Image caption Simba

Timu ya Etincelles ya Rwanda imekuwa ya kwanza kuyaaga mashindano ya CECAFA Klabu Bigwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame baada ya kufungwa kwa mara ya tatu mfululizo pale ilipofungwa na Red Sea ya Eritrea jumla ya magoli 4 – 1 katika mchezo wa awali ulifanyika katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Tanzania.

Katika mechi ya awali Etincelles ilifungwa na Zanzibar Ocean View 3-2 na baadae ikafungwa na Vital’o ya Burundi magoli 3-1. Katika mechi ya pili iliyochezwa katika uwanja huo huo wa Taifa mjini Dar es Salaam Simba ya Tanzania imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuifunga timu ya Ocean View ya Zanzibar goli 1-0 Goli pekee la Simba limefungwa na Amir Mrisho Maftah katika kipindi cha kwanza kwa shuti kali akiwa umbali wa mita 40 na kumshinda mlinda mlango wa Ocean view Abass Nassor Ali. Kabla ya kufunga goli hilo Amiri Mrisho Maftah alikosa penati baada ya mshambuliaji wa Simba Mussa Hassan Mgosi kufanyiwa faulo katika kisanduku cha kumi na nane.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalikuwa 1-0. Kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanjani kwa shauku ya ushindi ambapo zilishambuliana kwa zamu hata hivyo kukosekana kwa umakini wa washambuliaji wa Simba kulifawanya wakose magoli mengi hadi fulimbi ya mwisho matokeo yalikuwa ni yale yale 1-0. Kwa matokeo hayo Ocean View ya Zanzibar inaendelea kushika nafasi ya Kwanza kwenye kundi A ikufuatiwa na Vital'o ya Burundi nafasi ya pili ikiwa na pointi 4 sawa na Simba iliyopo nafasi ya tatu, Red Sea ya Eritrea nafasi ya tano ikiwa na pointi 3 na Etincelles ya Rwanda ya mwisho ambayo hadi sasa haijapata pointi hata moja. Bunamwaya Uganda itashuka dimbani kumenyana na timu El Mereikh ya Sudan siku ya Alhamisi katika mchezo wa awali utakaochezwa katika uwanja wa Dar es Salaam na baadae Yanga ya Tanzania itashuka dimbani kupambana na timu ya Elman ya Somalia katika mchezo wa pili wa kundi B .