Senegal waandamana kupinga mgao wa umeme

Maandamano yamezuka katika mji mkuu wa Senegal, Dakar na katika jiji la kusini la Mbour kutokana na ukosefu wa umeme. Jijini Dakar, majengo kadhaa ya serikali yalichomwa moto, zikiwemo ofisi za shirika la umeme la serikali - Senelec.

Image caption Maandamano Dakar

Majeshi ya usalama katika mji wa Mbour yalipiga mabomu ya machozi kutawanya maelfu ya waandamanaji.

Tatizo la ukataji umeme, ambao umedumu kwa saa 48 katika maeneo kadhaa, limekuja wiki moja tu baada ya kutokea maandamano dhidi ya rais.

"Mamia ya vijana walivamia ofisi za Senelec na kuzichoma moto," amesema mkazi mmmoja wa Dakar, Ismail Diop akikaririwa na Reuters.

Chupa zilizovunjwa, mabaki ya majengo na matairi yaliyochomwa moto vimetapakaa mitaani, amesema mkazi huyo.

Miaka mingi

Mjini Mbour, karibu kilomita 80 kusini mashariki mwa Dakar, ofisi za shirika la umeme pia zilishambuliwa. watu walioshuhudia walisema ofisi za Senelec zilivunjwa na magari yaliyoegeshwa nje kushambuliwa pia.

Senelec imeshindwa kutoa huduma ya umeme ya kuridhisha kwa miaka mingi.

Wiki iliyopita, kulikuwa na maandamano mjini Dakar, yaliyotokana na pendekezo la rais Abdoulaye Wade kutaka kubadilisha katiba.

Maandamano hayo yalikuwa ya kiwango ambacho hakijawahi kuonekana katika kipindi cha miaka 11 ya utawala wa Bw Wade.

Gharama za maisha

Rais huyo alitaka kupunguza kiwango cha asilimia kinachohitajia kushinda urais kutoka asilimia 50 hadi 25 ili kuepuka duru ya pili katika uchaguzi.

Wakosoaji wamesema marekebisho hayo ya katiba yamelenga kuhakikisha Rais Wade, ambaye ana umri wa miaka 85, anachaguliwa tena mwakani.

Bw Wade alingia madarakani katika uchaguzi wa kidemokrasia, lakini sasa anakabiliwa na ongezeko la hasira kutoka kwa wananchi kutokana na matatizo ya umeme ya kila siku na kupanda kwa gharama za maisha.