Ukame waikumba Pembe ya Afrika

Somalia Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Msomali akisubiri msaada

Baadhi ya maeneo ya Pembe ya Afrika yamekumbwa na ukame mbaya kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 60, umesema Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya watu milioni 10 wanadhaniwa kuathirika na hali hiyo katika eneo hilo.

Umoja wa Mataifa umetaja kuwa Somalia, Ethiopia, Djibouti na Kenya, ndio zipo katika hali mbaya.

Shirika la misaada la Save the Children limesema ukame na vita nchini Somalia ndio zimesababisha idadi kubwa ya watu kukimbilia Kenya, na inakadiriwa watu takriban 1,300 wanawasili kila siku.

Kambi tatu zilizopo Daadab nchini Kenya, zinahifadhi zaidi ya watu laki tatu, ingawa kambi hizo zilijengwa kuhifadhi watu 90,000.

Ukosefu wa mvua ulioanza mwishoni mwa mwaka 2010, sasa unaleta athari.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uratibu wa masuala ya kibinaadam (Ocha) imeonya kuwa hali inazidi kuwa mbaya, na idadi ya watu wanaohitaji misaada itaendelea kuongezeka.

Idadi ya walioathirika ni kubwa, inasema Ocha: watu milioni 3.2 nchini Ethiopia, milioni 3.2 nchini Kenya na milioni 3.2 nchini Somalia, na zaidi ya watu laki moja nchini Djibouti.

Kila mwezi, mwaka 2011, takriban Wasomali 15,000 walikimbia nchi yao, na kuwasili Kenya na Ethiopia, kwa mujibu wa Ocha.

Wakati mzozo wa Somalia ukiwa ndio hali halisi ya kila siku kwa miaka mingi, hali ya ukame ndio imewaumiza zaidi. Wengi wametembea kwa siku kadhaa, wamechoka, hali yao ya kiafya ni mbaya, na wanahitaji chakula na maji.