Bunge lapitisha mswada muhimu Ugiriki

Makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga mpango wa kuunusuru uchumi wa Ugiriki yameendelea mjini Athens kutwa nzima.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Raia wanapinga mpango huo ambapo kodi itaongezeka maradufu

Mabomu yaliotengenezwa na petroli yamekua yakilipukua jioni nzima, huku polisi wakutuliza ghasia wakiwarushia watu hao waliokusanyika nje ya jengo la bunge gesi za kutoa machozi.

Lakini licha ya vurugu hizo, mswada wa serikali uliochochea machungu haya yote ulipitishwa japo katika mazingira ya ushindani mkali.

Wabunge 155 waliunga mkono pendekezo hilo huku wengine 138 wakipinga. Leo wabunge watapiga kura tena kubadilisha sheria ili mpango huo utekelezwe.

Waziri mkuu George Papandreou amelenga kubana matumizi ya serikali ili ifikiapo mwaka wa 2015 watakuwa na hazina ya pauni bilioni 25.

Pamoja na hilo, amependekeza kupandisha kodi ili kuongezea kipato cha serikali, hatua iliochochea maandamano hayo nchini humo.

Lakini waziri mkuu Papandreou anasema mpango huo ukitibuka ni sawa na kuangamiza nchi hiyo.

Umoja wa ulaya umepongeza bunge kupitisha pendekezo hilo ambapo liki zingatiwa serikali ya Ugiri huenda ikafaulu kulipa malimbikizi ya madeni yake.

Hata hivyo bado kuna wale ambao hawaamini kuwa mpango huo utafaulu.

Serikali ya Ugiriki sasa inatarajia kupata mkopo wa euro billioni 110 kutoka kwa shirika la fedha duniani na umoja wa ulaya kutatua matatizo yake ya kiuchumi.