Muungano wa Afrika waishutumu Ufaransa

Kamishna Jean Ping Haki miliki ya picha AP
Image caption Kamishna Jean Ping

Kamishna wa tume ya Muungano wa Afrika Jean Ping amesema kuwa uamuzi wa Ufaransa kuwarushia silaha waasi wa Libya kutoka angani ni hatari na kuwa mtindo huo unahatarisha eneo zima.

Ameiambia BBC kuwa hatua hii huenda ikaitumbukiza Libya katika matatizo sawa na yale yanayoonekana katika nchi ya Somalia ambayo imekabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi.

Ufaransa imekiri kuwa iliwapa silaha wapiganaji wa Berber kwa kuzirusha toka angani katika milima ya kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli.

Wadadisi wanasema kuwa hatua hiyo huenda inakiuka vikwazo vilivyowekwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupinga silaha kupelekwa Libya.

Bw Ping alikuwa anazungumza kutoka Equatorial Guinea ambako viongozi wa Afrika wanakutana katika kikao cha kikele cha Muungano wa Afrika.

Suala la Libya inatarajiwa kupewa kipaumbele katika mkutano huo.

Bw Ping amesema kuwa mpango wa amani wa Muungano wa Afrika kwa Libya ulioafikiwa mwezi Marchi bado upo na unafaa. Mpango huu unahusu utaratibu wa amani unaonuiwa kufungua njia ya mazungumzo ya kisiasa.

Taarifa kuhusu Ufaransa kuwapa silaha waasi zilifichuliwa na gazeti la Le Figaro hapo jana.Gazeti hilo liliongeza kusema kuwa Ufaransa haikuwafahamisha wenzake katika kikosi cha kujihami cha Nato kuhusu hatua yake hiyo.

.

Taarifa hiyo imesema silaha hizo ni pamoja na makombora ingawa maafisa wa Ufaransa wanasisitiza na kuthibitisha kuwa silaha zilizorushiwa waasi hao zilikuwa ndogo ndogo.

Uwamuzi huu inaarifiwa uliafikiwa baada ya mkutano wa mwezi Aprili kati ya Rais Sarkozy wa Ufaransa na kiongozi wa wapiganaji wa waasi Jenerali Abdel Ifatah Younis.

Ufaransa imekuwa ikionesha wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mapigano haya ya Libya yalioanza mwezi February.

Waasi wameonekana kupiga hatua na wanatumai kuelekea Tripoli kutokea maeneo ya milimani ya Nafusa kilomita 65 kutoka mji mkuu huo.

Urusi na Uchina zimeshutumu mashambulio ya Nato, zikisema kuwa yamevuka mipaka ya azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1973 linaloruhusu hatua za kijeshi kuchukuliwa nchini Libya.

Hatahivyo Marekani inasema kuwa azimio la mwaka 1973 linaruhusu nchi kuwapa waasi silaha licha ya azimio la awali la mwaka 1970 ambalo liliiwekea Libya vikwazo vya silaha.