Sudan kuondoa majeshi kabla ya uhuru

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Kiongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir

Majeshi ya pande zinazozozana nchini Sudan yamekubaliana kuondoka katika mpaka wa kaskazini kusini, kabla ya uhuru wa Sudan wiki ijayo.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa Ethiopia yamekuja baada ya mapigano katika mipaka miwili ya maeneo ya Abyei na Kordofan Kusini, yaliyowalazimu watu wapatao 170,000 kukimbia makazi yao.

Majeshi hayo yakiondoka yatatakiwa kuacha sehemu yenye umbali wa kilometa 20 (maili 12) kutoka eneo la mapambano.

Mapigano hayo yamezusha hofu kuwa miaka 21 ya vita vya Kusini na Kaskazini vinaweza kuanza tena.

Makubaliano hayo yaliyofanyika chini ya uongozi wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki yanafuatia mengine kadhaa yalimaliza mapigano ya Abyei na Kordofan Kusini.

Waangalizi wa Kimataifa na vikosi vya kulinda amani vya UN vitasimamia makubaliano hayo.

Pande zote mbili zinaing'ang'ania Abyei; wakati mapigano ya Kordofan Kusini yanatokana na vikosi vya kaskazini kupigana dhidi ya kabila la Wanuba waliowasaidia waasi wa Kusini wakati wa vita vya

wenyewe kwa wenyewe lakini kwa sasa wamejikuta wakiwa upande wa Kaskazini.

Mwandishi wa BBC Peter Martell aliyeko mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba anasema makubaliano hayo si rahisi yakatekelezwa kama inavyosikika kwa sababu maeneo hayo bado yanagombewa na mipaka bado haijatengwa.

Anasema makubaliano haya yataleta faraja kwa wengi Juba lakini watakuwa makini kuhakikisha kuwa yanatekelezwa.

Jumanne ilikubaliwa kuwa wapiganaji wa zamani wa Sudan Kusini walioko Kordofan Kusini watatakiwa kujiunga na jeshi la Kaskazini au wanyang’anywe silaha.

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika yanahusisha pia jimbo jirani la Blue Nile ambalo lina wapiganaji wa zamani wa kusini. Hata hivyo limekuwa halina mgogoro wowote.

Makubalino yanataka pia kuwa zoezi la kuwanyang’anya silaha lisitumie nguvu.

Mapema wiki hii Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kupeleka vikosi 4,200 vya kulinda amani kutoka Ethipia katika eneo la Abyei baada ya makubaliano ya awali kulifanya lisiwe eneo la vita.

Pande hizo mbili bado hazijafikia muafaka namna zitakavyogawana utajiri wa mafuta baada ya Uhuru.

Asilimia 75% ya eneo la mafuta iko upande wa Kusini lakini mabomba ya mafuta yanaelekea kaskazini mpaka eneo la Bandari katika bandari ya Port Sudan iliyoko pwani ya bahari ya Shamu.

Kwa sasa mapatao yanatakiwa kugawanywa sawa kwa pande zote mbili.