Usalama unakabidhiwa kwa Afghanistan

Afghanistan imeanza utaratibu wa kuchukua madaraka ya usalama yenyewe, na jimbo la Banyan limekuwa la mwanzo kukabidhiwa na jeshi la NATO kwa polisi wa Afghanistan.

Haki miliki ya picha Steve Maccarry Magnum photos

Mawaziri wa Afghanistan na mabalozi wa nchi za nje walihudhuria sherehe hiyo katika jimbo la kati.

Mwandishi wa BBC nchini Afghanistan, anasema Bamiyan ni moja kati ya majimbo yaliyo salama kabisa nchini humo, lakini wakaazi wake wengi wanaogopa kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuzusha rushwa na usalama kupungua.

Na kamati ya bunge la Uingereza imelalamika vikali kuhusu jukumu walilopewa wanajeshi wa Uingereza, walipopelekwa Afghanistan awali, na kamati hiyo imeonya dhidi ya kuliondoa jeshi hilo haraka.

Wabunge wa kamati wanasema ikiwa wanajeshi zaidi ya mia chache watarudishwa nyumbani, basi mkakati wa jeshi la kimataifa nchini Afghanistan utachafuka, na kudhoofisha vikosi vitavyobaki. Janan Mosazai ni msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje ya Afghanistan.

Aliiambia BBC kwamba ni sawa kwa Waafghan wenyewe kuwa na dhamana ya usalama wao:

"Usalama wa Afghanistan ni jukumu la Waafghani wenyewe, na Rais Karzai amekuwa akieleza wazi wazi kwa miaka kadha sasa, kwamba dhamana hiyo lazima tuibebe sisi Waafghani.

Tunaishukuru jamii ya kimataifa, Marekani, Uingereza na washirika wengine wote, kwa kujitolea kwao kwa damu na mali, katika miaka kumi hii iliyopta.

Na tunatumai tutashirikiana kimkakati na jumuiya ya kimataifa, lakini usalama wa Afghanistan hatimaye ni jukumu la WaAfghani."