Murdoch anaomba msamaha

Tajiri anayemiliki vyombo vya habari kadha duniani, Rupert Murdoch, ameomba msamaha kwa wananchi wa Uingereza, kwa makosa yaliyofanywa na gazeti lake moja, News of the World.

Haki miliki ya picha PA

Gazeti hilo lilifanya udaku katika maelfu ya simu za mkononi za watu.

Msamaha huo umetolewa kama tangazo lilochapishwa kwenye magazeti kadha lenye kichwa cha maneno: "tunaomba msamaha", na ambalo limetiwa saini na Bwana Murdoch.

Anasema anaomba msamaha kwa makosa makubwa na kwa kuwaumiza watu walioathirika na udukuzi huo.

Mwandishi wa BBC anasema siyo mara nyingi kwa watu wakubwa duniani kuomba radhi hadharani.

Lakini tajiri huyo anayemiliki vyombo vya habari kadha, ilimbidi kufanya hivo, baada ya gazeti lake la Uingereza, lilokuwa likisomwa na watu wengi kabisa nchini, kugunduliwa kuwa likifanya udaku kwa kusikiliza ujumbe kwenye simu za maelfu ya watu.

Kati yao walikuwamo watu wa ukoo wa kifalme wa Uingereza, wachezaji sinema na waimbaji maarufu, na piya familia za wanajeshi waliouwawa vitani nchini Iraq na Afghanistan -- na hata simu ya msichana aliyeuliwa.

Katika barua yake Bwana Murdoch piya anasema kampuni yake ya News International, itachukua hatua zaidi kutatua maswala yaliyozuka kutokana na kashfa hiyo ya udukuzi kwenye simu.

Hapo jana, wakurugenzi wawili wa kampuni ya bwana Murdoch walijiuzulu.