Misaada inapitia kwa al-Shabaab

Mratibu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Mark Bowden, anasema msaada unatolewa katika baadhi ya makambi yaliyopewa idhini na kikundi cha wapiganaji wa Kiislamu, Al-Shabaab.

Bwana Bowden aliiambia BBC kwamba msaada unatolewa kwa kupitia kamati za Al-Shabaab, zinazohusika na ukame ambazo zinaendesha makambi hayo.

Bwana Bowden alisema ilibidi kufanya hivo, ingawa inajulikana kuwa Al-Shabaab ina uhusiano na Al-Qaeda, ikiwa msaada wenyewe unatolewa kufuatana na misingi ya utu, bila ya kuhusisha siasa.

Alisema ni lazima kuzidisha shughuli nchini Somalia katika miezi michache ijayo.