Utapia mlo unazidi Pembe ya Afrika

Mkuu wa shughuli za misaada ya dharua ya Umoja wa Mataifa, Lady Amos, ametoa wito kuchukuliwe hatua za haraka kupambana na utapia mlo uliosababishwa na ukame mkubwa katika Pembe ya Afrika.

Uhaba wa maji katika eneo hilo haukupata kuonekana tangu mwaka wa 1951 - na mashirika ya misaada yanasema watu milioni 10 wa Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia na Uganda wameathirika.

Lady Amos anasema msaada unahitajika haraka; na ikiwa hilo halikushughulikiwa katika majuma machache yajayo, basi hali itazidi kuwa mbaya.

Mashirika ya misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa tayari yanakutana na watoto zaidi wanaotapia mlo; na sasa wanaanza kuona hata watu wazima waliodhoofika kwa njaa.

Lady Amos anaeleza hasa matatizo ya kufikisha msaada katika sehemu za Somalia zilizokumbwa na vita baina ya kikundi cha wapiganaji cha Al Shabab na serikali inayosaidiwa na mataifa ya Magharibi.

Kuna tatizo piya la wasi wasi wa Marekani na wafadhili wengine, kuwa msaada usiwafikie wapiganaji wa Al-Shabab.

Lady Amos anasema matokeo ya wasi wasi huo, ni kuwa msaada kwa ajili ya Somalia, umepungua.