Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Ajali

Dereva mmoja nchini Marekani aliyekuwa akiendesha gari huku akiwa amelewa chakari aligona mtu aliyekuwa akitembea barabarani bila kujua kilichotokea.

Mtu huyo aliyegongwa alipasua kioo cha mbele na kuangukia kwenye kiti cha abiria ndani ya gari, bila hata dereva mlevi kugutuka kilichotokea. Dereva huyo aliposimamishwa na polisi umbali mfupi kutoka ilipotokea ajali hiyo jijini Houston, Texas, aliwaambia polisi kuwa alihisi kuwa amegonga kitu, lakini hakujua ni kitu gani.

Dereva huyo amekaririwa na mtandao wa myFox.com akisema wala hakuwa na habari ya ajali licha ya gari lake aina ya Mazda kuwa limepasuka kioo cha mbele na mtu aliyegongwa kuwa ameangukia ndani ya gari.

Dereva huyo John Onak atashitakiwa kwa kushindwa kusimama na kutoa msaada, na pia kwa kuendesha gari akiwa amelewa.

Polisi walimkuta mtu aliyegongwa akiwa na mguu mmoja tu, ingawa baadaye waliukuta mguu wake mwingine uliokatika katika barabara kuu kati ya Houston na Galveston, ambapo ajali hiyo ilitokea.

Tabia mbaya

Mwanamke mmoja nchini Marekani aliingia matatani baada ya kuwashambulia polisi na matiti yake wakati polisi wakijaribu kumkamata.

Polisi walikuwa wameitwa baada ya mama huyo aitwaye Stephanie Robinette kumfanyia vurugu mumewe.

Mume wa mwanamama huyo aliwaambia polisi kuwa mke wake alimpiga mara kadhaa kabla ya kukimbilia ndani ya gari na kujifungia.

Kituo cha televisheni cha WBNS kimeripoti kuwa polisi walipojaribu kumtoa ndani ya gari hilo, mama huyo aliwaonya kwa kuwambia kuwa yeye ni mzazi mwenye mtoto mdogo anayenyonya.

Polisi walipopuuza onyo lake hilo, mwanamama huyo alitoa ziwa lake la kulia na kuanza kuwanyeshea polisi hao kwa maziwa.

Hatimaye, wakiwa wamelowa na maziwa polisi hao walifanikiwa kumtoa Bi Robinette ndani ya gari, na kumfunglia mashitaka ya ghasia nyumbani, kushambulia, kuzuia kazi ya polisi na kugoma kukamatwa.

Hakuna mashtaka ya moja kwa moja kuhusiana na maziwa yametajwa.

Wakwe wakikukataa

Kwa wasichana wanaotaka kuolewa, bila shaka suala la kuwa na uhusiano mzuri na wakwe huwa gumu kidogo, lakini kwa msichana mmoja hapa Uingereza ugumu huo huenda umekithiri.

Bi Heidi Withers ambaye amepanga kufunga ndoa na mchumba wake, Freddie, walikwenda kuona wazazi wa Freddie, na mara moja mama yake Freddie hakupendezwa na mchumba alioletwa na mwanaye.

Baada ya wachumba hao kuondoka Mama yake Freddie, aitwaye Carolyne Bourne alituma barua pepe kwa mkwe wake akilalamika jinsi alivyoonesha tabia mbaya.

Katika barua pepe hiyo, iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho -- Ukosefu wa adabu, mama huyo amemchambua vilivyo mkwe wake mtarajiwa.

Amekosoa jinsi mchumba wa mwanae anavyokula chakula, na kusema hata vichekesho alivyokuwa akitoa havina maana na wala havichekeshi.

"Lazima mtu amfunze adabu" imekaririwa sehemu ya barua pepe hiyo. Aidha mama huyo ameponda mipango ya harusi ambayo imepangwa kufanyika katika jumba la kifahari, akisema binti huyo hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

"Huweza kufanya harusi katika jumba la kifahari, kama sio lako, Hiyo ni kupenda maisha ya kifahari" amesema mama mkwe huyo.

Mume wa mama mkwe huyo amekataa kusema lolote kuhusiana na sakata hilo, na hata bwana harusi naye amegoma kusema lolote kuhusiana na matamshi ya mama yake.

iphone

Haki miliki ya picha Reuters

Wiki kadhaa baada ya mchina mmoja kuuza figo yake ili kununua iPad, mchina mwingine wa kike safari hii amejitokeza kutoa mwili wake kwa mwanaume atakayemnunulia simu aina ya iPhone 4, toleo jipya kabisa.

Gazeti la Korean Herald limeripoti kuwa msichana huyo aliyetajwa kwa jina la Jiulinghou -- ambayo maana yake kwa kichina ni kama kizazi cha mwisho, aliandika katika mtandao wa Weibo -- yaani Tweeter ya Kichina -- kuwa ni ndoto yake kuwa na simu aina ya iPhone 4, lakini hana uwezo na baba yake kakataa kumnunulia.

Katika mtandao huo msichana huyo ambaye ni bikra aliweka pia na picha yake, pamoja na taarifa fupi kuhusu maisha yake, akisema yuko tayari kuuza usichana wake kwa yeyote atakayemnunulia iPhone.

Mtandao wa Courier Mail haukusema iwapo msichana huyo alifanikiwa au la.

Kujifungua ghafla

Haki miliki ya picha PA

Mwanamama mmoja hapa Uingereza alijifungua mtoto wa kiume, muda mfupi tu baada ya kuambiwa kuwa ana uja uzito wa miezi tisa.

Msichana huyo aitwaye Sarah ameliambia gazeti la Daily Mail kuwa hakugundua kuwa ana uja uzito wowote, kwa kuwa, alikuwa alikuwa akienda kazini kama kawaida, na kwamba hata mwili wake hakuongezeka.

"Nilipoteza uzito, nikawa mwembaba" amesema Sarah. Mwanaye huyo amebaye amempa jina la Stanley, alizaliwa wiki mbili baada ya kukamilika kwa miezi tisa.

Anasema alikuwa akihisi maumivu ya tumbo, lakini alidhani ni maumivu ya kawaida tu.

Siku ya siku baada ya kutoka kazini, Sarah amesema maumivu zaidi, na kulazimika kupiga simu kuita gari la kubebea wagojwa.

Madaktari katika gari la wagonjwa mara moja walitambua kuwa msichana huyo ni mja mzito.

Haraka haraka walimpakiza ndani ya gari, lakini hata hivyo hawakuweza kufika hospitali, Sara alijifungua ndani ya gari.

"Yaani mambo yalitokea haraka "amesema bi Sarah na kuongeza "Mara nikamsikia daktari akisema, naona nywele za mtoto"

Na kwa Taarifa Yako....... Mwayo mmoja hudumu kwa takriba sekunde sita

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa..