Uturuki yatambua waasi wa Libya

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mazoezi ya waasi Libya

Uturuki imetambua Baraza la Mpito la Kitaifa kama waakilishi wa kweli wa raia wa Libya.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema ni wakati sasa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kuondoka.

Uturuki imeahidi kutoa msaada wa dola milioni $200m kwa waasi, hii ni zaidi ya dola milioni $100m walizotangaza kutoa mwezi uliopita.

Waasi wamekataa juhudi za Muungano wa Afrika za kuanzisha mazungumzo kati yao na serikali mjini Tripoli.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kanali Gaddafi

Msemaji wa waasi Abdel Hafiz Ghoga amesema: "tumekataa mpango huo.Haukutaja kuondoka kwa Gaddafi,watoto wake na washirika wake wakuu."

Lakini kiongozi wa baraza hilo la mpito Mustafa Abdul Jalil amekubali kuwa Kanali Gaddafi anaweza kuishi maisha yake ya kustaafu nchini Libya iwapo tu ataacha madaraka.

" Kama njia ya kuleta suluhu,tumemwambia ajiuzulu na aamrishe majeshi yake kuondoka kwenye kambi na ngome zao, na alafu anaweza akaamua kama ataishi Libya au nje ya Libya," aliambia shirika la habari la Reuters.

"Kama angependa kuishi Libya, tutaamua atakaa wapi na sehemu itakuwa chini ya uangalizi wa kimataifa.Na kutakuwa na uangalizi wa kimataifa kwa kila anachofanya."

'Suluhisho la kudumu'

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki alikutana na Bwana Jalil mjini Benghazi, ngome kuu ya waasi mashariki mwa Libya,kabla ya kuhutubia waandishi wa habari katika mji huo.

"Niko hapa kuungana na watu wa Libya. Haki yao ya kimsingi lazima itimizwe,lazima kuwe na suluhisho la kudumu kwa mzozo huu,hilo litawezekana tu kukiwa na suluhisho la kisiasa katika yale ambayo watu wa Libya wanataka.

"Tunaona Baraza la Mpito la Kitaifa kama waakilishi wa kweli wa watu wa Libya na watakaofikia malengo ya watu wa Libya."

Waandishi wanasema safari ya Bwana Davutoglu mjini Benghazi ni ishara kuwa Uturuki - nchi yenye uwezo mkubwa kwenye eneo hilo na mwanachama wa Nato na ambayo kwanza ilipinga hatua ya kijeshi inayoongozwa na nchi za magharibi ya kuwaunga mkono waasi wa Libya - kuwa sasa inaunga mkono wapinzani wa Libya.