Rais wa Venezuela ahutubia taifa

Rais Hugo Chavez Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais Hugo Chavez akiwahutubia wafuasi wake

Rais wa Venezuela Hugo Chavez amehutubia maelfu ya watu mjini Caracas baada ya matibabu nchini Cuba.

Wafuasi wa rais Hugo Chavez walimshabikia wakati alipowaonyesha bendera ya Venezuela kutoka kwa roshani ya kasri yake na kusema kuwa afya yake itaimarika. Rais Chavez amewahutubia maelfu ya wafuasi mjini Caracas baada ya kupata matibabu ya saratani nchini Cuba.

Bwana Chavez,mwenye umri wa 56,amekuwa nchini Cuba tangu Juni 8,alikofanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe uliokuwa na saratani.

Nimerudi!

Alisema kuwa hatoweza kushiriki katika sherehe za kuadhimisha miaka 200 ya uhuru wa Venezuela kutoka kwa Uhispania siku ya Jumanne.

Lakini atafuatilia sherehe hizo akiwa kwenye kasri ya rais,alisema.

Akiwa amevaa magwanda yake ya kijeshi na kofia nyekundu,Bwana Chavez kwanza aliongoza umati huo kuimba wimbo wa taifa wa Venezuela.

" Nimerudi," alisema,akishukuru wale wanaomuunga mkono. " Hii ndiyo dawa bora kwa ugonjwa wowote ule."

Hakuna tena uvumi.

Chavez haondoki!

Akisimama bila kusaidiwa,Bwana Chavez alizungumza kwa muda wa dakika 30 bila kuangalia popote.

Maelfu ya wafuasi waliokuwa wamevaa mavazi mekundu,walisema: "Hapana! Chavez haondoki!"

Awali,Bwana Chavez alisema amekuwa "na wakati mgumu" nchini Cuba lakini kwamba sasa anaendelea kupata nafuu.

Bwana Chavez, ambaye ameongoza Venezuela kwa miaka 12 na hata kunusurika jaribio la mapinduzi mwaka 2002,aliambia Televisheni ya taifa kuwa ana utaratibu kamili wa matibabu "anatumia dawa,anatakiwa kupumzika,na kula vyakula maalum".

Kumekuwa na uvumi kuhusu hali ya afya ya Bwana Chavez baada ya kuondoka Venezuela zaidi ya wiki tatu zilizopita kwa kile maafisa walisema ni kufanyiwa upasuaji.