Fifa kutoka adhabu kali asema Blatter

Rais wa shirikisho la mchezo wa soka duniani Fifa Sepp Blatter, amesema mtu yeyote atakayepatikana na kosa katika kashfa ya kupanga matokeo ya mechi za timu ya taifa ya Zimbabwe atapigwa marufuku ya kutoshiriki katika shughuli zozote za soka maishani mwake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa FIFA Sepp Blatter

Wachezaji wa timu ya taifa akiwemo naodha wa timu hiyo, Method Mwanjali waliiambia tume iliyoundwa na shirikisho la mchezo wa soka nchini Zimbabwe, Zifa kuwa walilipwa ili kupoteza mechi zao wakati wa ziara yao barani Asia mwaka wa 2009.

Maafisa wa tume ya kupambana na ufsadi wa Fifa wanatarajiwa kuzuru Zimbabwe hivi karibuni ili kushauriana na maafisa wa Zifa na polisi kabla ya kukamilishi uchunguzi wao kuhusiana na kashfa hiyo.

Blatter aliyasema hayo wakati wa ziara yake fupi nchini Zimbabwe, kutoka kwa mkutano wa Kamati ya kimataifa ya michezo ya olimpiki IOC uliofanyika mjini Durban Afrika Kusini.

Fifa kutoa adhabu kali zaidi

"Hatuwezi kuingilia kati suala hili kwa haraka, ni lazima tupate idhini kutoka kwa mataifa husika na wakati watu watapatikana na hatia, sisi tutawapiga marufuku ya maisha" alisema Blatter.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mchezaji wa timu ta Taifa ya Zimbabwe Knoledge Musona

"Hatutawaruhusu tena watu hao kujihusisha na usimamizi wa mchezo wa soka, ikiwa wao ni maafisa wa Zifa au wachezaji, wataadhibiwa vikali na kwa mujibu wa sheria" aliongeza Blatter.

Ushahidi uliotolewa na wachezaji kwa tume hiyo iliyoundwa na Zifa, unadai kuwa maafisa wa Zifa walishirikiana na raia mmoja wa Singapore, Raj Perumal, kuwahonga wachezaji hao ili wapoteze mechi zao dhidi ya Syria na Thailand.

Uchunguzi wa pili uliangazia ziara za awali za timu hiyo ya taifa ya Zimbabwe barani Asia, ambako pia walipoteza mechi zao dhidi ya mataifa yanayoorodheshwa ya chini zaidi katika msimamo wa nchi bora duniani.