Nataka kuihama Man City-Tevez

Mshambulizi Carlos Tevez anasema anataka kuondoka Manchester City kutokana na sababu za kifamilia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Carols Tevez akisherekea bao alilofunga

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina amesaidia Manchester City kumaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita kwenye ligi kuu ya England na kuweza kufuzu kwa ligi ya klabu bingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27,alijiunga na City kutoka kwa wapinzani wao wa mji wa Manchester United mwaka 2009, amesema hawezi kuendelea kuishi kaskazini magharibi,bila binti zake wawili.

Kwa nini ataka kuondoka?

" Nahitaji kuwa karibu nao na kuwa na muda nao," Tevez alisema katika taarifa.

" Kuishi bila watoto wangu Manchester imekuwa changamoto kubwa kwangu.Kila ninachofanya,nafanya kwa ajili ya binti zangu.

Image caption Carols Tevez akichezea timu yake ya taifa ya Argentina

" Nataka wawe na furaha kwa kuwa maisha yangu ni kwa ajili yao sasa. Nahitaji kuwa mahali ambapo wao wanaweza kuishi vizuri.

" Natumai kuwa watu wanaelewa mazingira haya magumu ambayo nimekuwa katika miezi 12 iliopita,hasa ukizingatia familia yangu."

Tevez, ambaye alitia saini kandarasi ya miaka mitano na Manchester City kwa kiasi cha pauni za Uingereza milioni £25.5m kutoka Old Trafford,alishukuru uongozi wa timu ya City kwa ushirikiano wao na kuomba mashabiki waelewe masuala yake binafsi kwa sasa.