Marufuku yaondolewa na al-Shabab Somalia

Al-Shabab

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab nchini Somalia limeondoa marufuku iliyowekwa dhidi ya mashirika yote ya kigeni ya misaada, hasa wakati huu eneo hilo la upembe wa Afrika linakumbwa na ukame mbaya kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 60.

Al-Shabab iliyapiga marufuku mashirika yote ya misaada ikiyashutumu kuwa yanapinga dini ya Kiislamu

Kwa sasa kundi hilo linasema kuwa mashirika yote ya misaada ya Kiislamu na yasiokuwa ya Kiislamu yanaweza kutoa misaada ya dharura bora tu yasiwe na azma nyengine mbovu.

Karibu robo ya Wasomali wamekabiliwa na ukame ambapo wengi wamekimbilia nchi jirani.

Msemaji wa al-Shabab Sheikh Ali Mohamud Rage amesema kundi hilo limeunda kamati itakayoshughulikia suala la ukame na kuwa mashirika ya misaada itabidi yashirikiane na kamati hiyo.

Aibu Wadadisi wanasema hatua hii huenda imechochewa na izara ambayo al-Shabab imepata baada ya maelfu ya Wasomali kuondoka kutoka maeneo inayotawala wakitafuta chakula.

Hatahivyo bado haijajulikana wazi mashirika hayo yatafanya kazi vipi kwa kuwa al-Shabab inataka yapate idhini yake kwanza.

Al-Shabab inatawala eneo kubwa la kusini na Somalia ya Kati.

Kundi hilo la al-Shabab linapigania utawala wa Kiislamu nchini Somalia na awali liliyaonya mashirika ya misaada mwaka 2009 yasifanye kazi na serikali ya mpito, ambayo inatawala sehemu za mji mkuu wa Somalia.

Idadi ya watu milioni 12 katika upembe wa Afrika wamekabiliwa na ukame wa mwaka huu.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema zaidi ya asili mia 50 ya watoto kutoka Somalia wanaoingia nchi jirani ya Ethiopia wanautapia mlo.

Kwa mujibu wa maafisa wanawashughulikia wakimbizi hao, watoto wadogo wanakufa wakiwa njiani ama siku moja baada ya kuwasili katika kambi hizo za wakimbizi.