Fifa yajipanga kusikiliza kesi ya Hammam

Kamati ya Fifa ya maadili itakutana tarehe 22 na 23 mwezi huu wa Julai kusikiliza shauri dhidi ya Mohamed bin Hammam, ambaye amesimamishwa kutokana na tuhuma za rushwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mohamed Bin Hammam

Anakabiliwa na tuhuma za rushwa, ikiwemo madai kwamba "alinunua" kura za kuandaa Kombe la dunia mwaka 2022 kwa Qatar, madai ambayo amekanusha.

Uchunguzi umekamilika na ripoti imepelekwa kwa Bin Hammam ambaye ni rais aliyesimamishwa wa Shirikisho la Sola la Asia.

Maafisa wa Umoja wa Soka wa nchi za Carrebean (CFU) Debbie Minguell na Jason Sylvester pia shauri lao litasikilizwa siku hiyo.

Minguell na Sylvester walisimamishwa pamoja na makamu wa Rais wa Fifa Jack Warner, ambaye hachunguzwi tena baada ya kuamua kujiuzulu shughuli zote za soka.

Mashtaka yanahusu mkutano wa vyama 25 vilivyo chini ya CFU mwezi wa Mei, ambapo inatuhumiwa rushwa ya dola 40,000 zililipwa na kwa kila mjumbe ambapo Bin Hammam wakati huo alikuwa katika kampeni za kuwania urais wa Fifa.

"Kamati ya maadili ya Fifa itakutana tarehe 22 na 23 mwezi wa Julai kusikiliza shauri la Mohamed bin Hammam, Debbie Minguell na Jason Sylvester, ambao awali walisimamishwa na kamati hiyo tarehe 29 mwezi wa Mei 2011, wakituhumiwa kukiuka maadili ya Fifa na kanuni za nidhamu za Fifa," taarifa ya Fifa ilieleza.