Liverpool yamkosa Downing wa Aston Villa

Dau walilotoa Liverpool la paundi milioni 15 kwa ajili ya kumchukua Stewart Downing limekataliwa na Aston Villa.

Image caption Stewart Downging

Inaaminika Villa wanashikilia walipwe paundi milioni 20 ili wamuachie winga huyo mwenye umri wa miaka 26.

Downing, aliyetokea Middlesbrough mwaka 2009 kwa kitita cha paundi milioni 12, mazungumzo yake ya mkataba yamekwama na meneja Alex McLeish inaonekana yupo tayari kumuachia aondoke.

Mchezaji huyo pia amehusishwa pia kujiunga na klabu ya Arsenal, lakini Liverpool wanaonekana ndio watafanikiwa kumsajili.

Bosi wa Liverpool Kenny Dalglish nia yake kubwa ni kuimarisha kikosi chake kufuatia timu hiyo kushika nafasi ya sita msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Soka ya England na tayari amefanikiwa kumchukua kiungo wa Sunderland Jordan Henderson.

Dalglish kwa sasa dira yake ameielekeza kwa Downing, ambaye anaonekana ataongeza kasi na muelekeo kwa Liverpool ambayo ilionekana kukosa ubunifu na mbinu msimu uliopita.

Downing huenda anaamini kwenda kwake Anfield kutamsaidia pia kuwa miongoni mwa wachezaji wa kwanza wa kikosi cha kawaida cha timu ya taifa ya England - lengo ambalo aliliweka hivi karibuni.

Licha ya kucheza mech 27 za timu yake ya taifa, Downing hivi karibuni alikiri: "Ninajiimarisha upya katika nafasi yangu kimataifa. Nimekuwa nikiitwa na kuondolewa katika kikosi cha timu ya taifa tangu nilipoanza kuichezea mara ya kwanza."

Pia aliesema msimu uliopita alipokuwa na Villa ulikuwa si wa kupendeza, walimaliza nafasi ya tisa na ingawa Villa wanaye meneja mpya McLeish, klabu hiyo inaingia katika kupindi cha mpito.

Mashabiki wengi wa Villa walipinga kuingia kwa meneja McLeish aliyetokea Birmingham na iwapo Downing ataondoka Villa Park, kufuatia kuhama kwa Ashley Young aliyejiunga na Manchester United, huenda hali ikawa si shwari.