Boko Haram yashambulia tena Nigeria

Boko Haramu

Mlipuko na ufyatulianaji risasi umesikika kaskazini mwa Nigeria katika mji wa Maiduguri-ngome ya wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi, wapiganaji wa Boko Haram waliurushia bomu msafara wa jeshi na kuwajeruhi maafisa watatu.

Baadae wanajeshi nao walikabiliana na wanamgambo hao kwa bunduki katikati mwa mji wa Maiduguri.

Mwandishi wa BBC Bilkisu Babangida akiwa katika mji wa Maiduguri anasema mji huo sasa umezingirwa na wakazi hawatoki nje.

Wapiganaji hao wa Boko Haram wanasema wanapigania utawala wa Kiislamu na vile vile wanafanya kampeini kupinga shughuli zote zenye uhusiano na mataifa ya magharibi.

Watu wasiopungua 40 wameuawa mjini Maiduguri katika kipindi cha siku kumi zilizopita, mauwaji hayo yamehusishwa na wanamgambo hao wa Boko Haram.

Mkuu wa kikosi cha jeshi huko Maiduguri Meja Jenerali Jack Nwaogbo ameiambia BBC kuwa maafisa wake wamekuwa wakilengwa na wapiganaji hao wakati wanapiga doria.

Maeneo ya burudani yanayouza pombe ambayo hutembelewa sana na wanajeshi na polisi, yamekuwa yakilengwa na Boko Haram.

Mwandishi wetu anasema mlipuko huo uliotokea saa moja asubuhi za Nigeria katika eneo la Abba Ganaram lililokuwa ngome ya kundi hilo kabla halijavamiwa na vikosi vya usalama.

Mapigano inasemakana yamefanyika karibu na kasri ya Shehu wa jimbo la Borno ambaye ni kiongozi wa waislamu anayeheshimiwa sana katika jimbo hilo.

Mwandishi wetu anasema walioshuhudia walimwambia kuwa magari yalioegeshwa karibu na eneo hilo yalishambuliwa wakati wa mapambano hayo.

Wanamgambo inasemekana wamekimbilia maeneo jirani na wanajeshi kwa sasa wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba.

Maduka na soko zimefungwa na watu wanahofu ya kutoka majumbani kwao.

Miaka miwili iliyopita vikosi vya usalama vya Nigeria vilikabiliana vikali na Boko Haram, na kuishambulia ngome yake na vile vile kumuua kiongozi wao Mohammed Yusuf alipokuwa korokoroni.

Badala ya kutoeka kabisa kundi hili limerejea tena na kuapa litalipiza mauwaji ya kiongozi wake.

Watu kadhaa wameuawa wengi wao maafisa wa usalama na wanasiasa na pia mhubiri mmoja mkristo na viongozi kadhaa wa Kiislamu walioshutumu kundi hilo la Boko Haram.

Kundi hilo pia lilishambulia makao makuu ya polisi katika mji mkuu wa Abuja hivi majuzi.