Yanga yafuzu hatua ya nusu fainali

Image caption Yanga, Tanzania

Timu ya Yanga ya Tanzania leo hii imesonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, al maarufu Kagame Cup.

Ni baada ya kuiondoa timu ya Red Sea ya Eritrea kwa njia ya mikwaju ya penati 6 - 5 katika mechi ya kukata na shoka ya robo fainali iliyomalizika jioni hii.

Mechi hiyo ilibidi kuamuliwa kwa mikwaju ya penati baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika bila kumpata mshindi kwani hadi filimbi ya mwisho matokeo yalikuwa 0 - 0.

Nurdini Bakari wa Yanga ndiye aliyeipeleka timu yake katika hatua ya nusu fainali baada ya kupata penati ya mwisho.

Hii ni mechi ya pili ya robo fainali kuamuliwa kwa mikwaju ya penati kwani hapo jana timu ya Al Mereikh ya Sudan nayo iliondoa ulinzi ya Kenya kwa njia hiyo hiyo ya mikwaju ya penati.

Hapo awali katika mechi ya kwanza ya robo fainalii iliyochezwa leo timu ya St. George ya Ethiopia nayo imefanikiwa kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga timu ya Vitalo ya Burundi kwa jumla ya magoli 2 - 0.

Kocha wa Vitalo ya Burundi Mnyarwanda Younde Kagabo amekiri kwamba timu yake ilizidiwa kiufindi na St. George.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga ya Tanzania watakutana na St. George ya Ethiopia siku ya Ijumaa.

Siku ya Alhamisi kutakuwa na mechi ya kukata na shoka ya nusu fainali ambapo Simba ya Tanzania wanaojulikana hapa Tanzania “Wekundu wa Msimbazi” wataingia uwanjani kumenyana na Al Mereikh ya Sudan.