Kesi dhidi ya LRA Uganda yaanza

Kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita dhidi ya kamanda wa kundi la waasi la Uganda la Lord's Resistance Army (LRA) imeanza mjini Gulu Kaskazini mwa nchi hiyo.

Thomas Kwoyelo, alifikishwa kwenye mahakama ya kitengo cha uhalifu wa kimataifa wa Uganda, miaka miwili baada ya kukamatwa kwake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Askari wa LRA

Shirika la habari la AFP limesema, alikana kuhusika na makosa 53 ya mauaji, utekaji nyara, uharibifu wa mali na kusababisha majeraha.

Waasi wa LRA wanajulikana kwa kulazimisha watoto wa kiume kupigana na kutumia watoto wa kike kuwa watumwa wa ngono.

Msamaha umekataliwa

Kundi hilo limeorodheshwa na Marekani kuwa kundi la kigaidi.

AFP imeripoti kuwa katika ufunguzi wa kesi hiyo, Jaji mkuu wa Uganda Yorokamu Bamwiine alisema: "raia wa Uganda na jumuiya ya kimataifa inahisi haki lazima itekelezwe na ndilo litakalofanyika."

Serikali mwanzo ilikataa ombi lake la kusamehewa.

Alikamatwa wakati wa uvamizi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 2009.