Saa chache kuelekea Uhuru Sudan Kusini

Haki miliki ya picha afp
Image caption Wasudani Kusini katika sherehe za kuzaliwa Taifa jipya

Sudan Kusini inahesabu saa chache ili kuwa Taifa jipya kabisa kuzaliwa duniani Jumamosi ya Julai 9.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir na wageni wengine mashuhuri kutoka kote duniani watahudhuria sherehe hizo zitakazofanyika katika mji mkuu Juba.

Zaidi ya asilimia 99 ya Wasudan Kusini walipiga kura kujitenga na Sudan Kaskazini katika kura ya maoni iliyofanyika mwezi Januari.

Kura hizo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2005 kumaliza miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha watu 1.5 milioni kufa.

Nchi mpya ya Sudan itakuwa na utajiri wa mafuta lakini itakuwa moja ya nchi maskini kabisa duniani kutokana na mapigano ya muda mrefu.

Sherehe zitaanza baada ya saa sita usiku saa za Sudan (2100 GMT) kwa kuhesabu dakika chache kufikia saa kamili ya kuwanza kwa siku wakitumia saa kubwa katikati mwa Juba.

Mwandishi wa BBC Will Ross anasema katika kuelekea kwenye tukio hilo la kihistoria, vituo vya redio vimekuwa vikipiga wimbo mpya wa Taifa la Sudan Kusini.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Mapema wiki hii Bw Bashir aliahidi kuiunga mkono Sudan Kusini na kusema kuwa anataka Taifa hilo jipya kuwa ‘salama na lililotengamaa.

"Tutawabariki ndugu zetu wa Kusini nchini mwao na tunawatakia mafanikio" alisema Bw Bashir, aliyekubaliana na mkataba wa amani na chama cha Sudan People's Liberation Army (SPLA).

Lakini ameonya kuwa ‘Uhusiano wa kindugu’ utategemea na mipaka salama na kutoingilia masuala ya nchi jirani (Kusini au Kaskazini)

Kulikuwa na wasiwasi huenda vita vingezuka tena baada ya mapigano mapya ya hivi kribuni katika maeneo ya mpakani Abyei na Kordofan Kusini ambayo yalilazimisha watu 170,000 kukimbia makazi yao.

Hata hivyo makubaliano tofauti ya wiki za hivi karibuni na kuondoa vikosi kwenye mipaka kumerejesha hali ya utulivu.

Rebecca Garang, mke wa hayati John Garang aliyeongoza waasi wa Sudan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe , ameiambia BBC kuwa watu wake hawana matatizo na watu wa Kaskazini isipokuwa serikali yao.

"Kuna rafiki zetu wengi tu ambao walikufa wakati w vita lakini tuko hapa kwa ajili ya damu yao," alisema.

Muhimu kuhusu Sudan Kusini

  • Idadi ya watu: 7.5-9.7 milioni
  • Ukubwa: 619,745 kilometa za mraba (239,285 maili), kubwa kuliko Uhispania na Ureno zikijumuishwa pamoja.
  • Lugha kuu: Kiingereza, Kiarabu (zote ni rasmil), Kiarabu cha Kijuba, Kidinka
  • Dini: Za kijadi/asili, Wakristo kidogo
  • Biashara ya nje: Mafuta
  • Moja ya nchi maskini kabisa duniani: Idadi kubwa ya vifo vya akina mama wajawazito; watoto chini ya miaka 13 hawasomi; 84% ya wanawake hawajui kusoma na kuandika.
  • Uhusiano na Sudan: Kugawana madeni na mafuta ; migogoro ya mipaka; uraia
  • Usalama: Takriban vikundi saba vya waasi

Changamoto za mbele

Wakati huohuo, Marekani imeitaka serikali ya Bw Bashir kuyaruhusu majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani kuendelea kubakia kaskazini, kufuatia vitisho kutoka Khartoum kuyafukuza kutoka majimbo ya Kaskazini ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

"Ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kuruhusiwa kulinda amani kikamilifu katika maeneo hayo kwa kipindi kirefu zaidi," alisema Susan Rice, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Mwandishi BBC anasema kuifanya Sudan ya Waislam Kaskazini na Kusini kuwa tulivu kwa muda mrefu baada ya sherehe kuisha itakuwa ni changamoto kubwa.

Pande zote mbili lazima zikamue juu mambo kama kuweka mpaka mpya na namna ya kugawana madeni na utajiri wa mafuta.

Wachambuzi wanasema kipaumbele kwa Khartoum kitakuwa kufanya mazungumzo juu ya mkataba mzuri wa mapato ya mafuta kwa sababu visima vingi viko Kusini.

Kwa sasa, mapato hayo yanagawanwa sawa kila upande.

Haki miliki ya picha other
Image caption Sudan Kusini ina utajiri wa mafuta

Khartoum ina nguvu kwa sababu mabomba mengi ya mafuta yanaelekea Kaskazini kwenye bandari ya Port Sudan iliyoko bahari ya Sham

Uraia pia ni suala ambalo bado halijafanyiwa maamuzi.

Kwa mujibu wa redio ya Taifa Sudan, uraia wa Wasudan Kusini wanaoishi kaskazini umekwishafutwa.

Mapema wiki hii, maelfu ya wafanyakazi Wasudani Kusini wanaofanya kazi kaskazini walilazamika kuacha kazi zao kabla ya kugawanyika.