Bendtner, Almunia 'waachwa' na Arsenal

Mshambuliaji wa Arsenal Nicklas Bendtner na golikipa Manuel Almunia wanafanya mazungumzo na vilabu vingine katika hatua ya kuondoka Emirates.

Image caption Nilkas Bendtner

Wawili hao wameachwa na timu ya wachezaji 23 wanaokwenda barani Asia kucheza mechi za kabla ya msimu.

Msemaji mmoja wa Arsenal amethibitisha taarifa hizi akisema wachezaji hao wawili wanafanya mazungumzo ya kuondoka Arsenal.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger anatarajiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala la uhamisho wa wachezaji siku ya Jumatatu.

Image caption manuel Almunia

Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas, ambaye amehusishwa vikali na kuhamia Barcelona ya Uhispania, pia hatosafiri na timu kwa kuwa anafanyiwa matibabu ya msuli.

Emmanuel Eboue pia hatosafiri akisumbuliwa pia na tatizo la misuli.

Hata hivyo, kiungo Samir Nasri ambaye ananyatiwa na Manchester United, Manchester City na Chelsea atasafiri na kikosi hicho.

Arsenal inakwenda Malaysia kupambana na All Star XI kabla ya kwenda kucheza na Hangzhou Greentown ya Uchina.