Michael Essien aumia goti mazoezini

Kiungo wa Chelsea Michael Essien ameumia goti alipokuwa mazoezini.

Image caption Michael Essien

Taarifa ya klabu hiyo imesema: "Michael ameumia goti la mguu wake wa kuume mazoezini wiki hii.

"Atafanyiwa uchunguzi siku chache zijazo kutambua ukubwa wa tatizo lake. Hadi tutakapopata matokeo kamili, kwa sasa klabu haitakuwa na la kuongeza."

Essien mwenye umri wa miaka 28, mwaka 2008 hakucheza soka kwa muda wa miezi sita baada ya kuumia goti.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana pia alishindwa kuiwakilisha nchi yake katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini kutokana na kuumia goti na kuumia kwake hivi sasa kunaonekana ni pigo kwa meneja mpya wa Chelsea Andre Villas-Boas, ambaye yumo katika kukinoa kikosi chake kwa ajili ya ziara ya Mashariki ya Mbali, ambapo timu hiyo itashiriki katika mashindano ya Kombe la Asia.

Wakati huo huo Chelsea imemtangaza Michael Emenalo kuwa mkurugenzi mpya wa michezo.

Emenalo alikuwa mwalimu msaidizi katika kikosi cha kwanza msimu uliopita, anachukua nafasi iliyoachwa na Ray Wilkins aliyehama klabu hiyo.

Mkurugenzi huyo mpya wa michezo kazi yake kubwa itakuwa ni katika mtandao wa kutafuta wachezaji wapya na maendeleo ya mipango ya wachezaji vijana na hali kadhalika kumsaidia Villas-Boas.