Viongozi waahidi kusaidia Sudan Kusini

Viongozi duniani wameahidi kulisadia taifa jipya kabisa duniani la Jamhuri ya Sudan Kusini.

Haki miliki ya picha afp
Image caption Raia wa Sudan Kusini

Marekani, Uchina, Urusi, Uingereza, Ujerumani, Nigeria na mataifa mengine mengi yalituma ujumbe wa pongezi na uungaji mkono kwa Sudan Kusini.

Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta, nchi hiyo mpya ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.

Jumamosi maelfu ya wananchi wa Sudan Kusini walikusanyika kushuhudia kupandishwa kwa bendera mpya ya nchi hiyo kuashiria kupata uhuru wake, katika mji mkuu Juba.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-moon walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria shughuli hiyo.

Sudan Kusini limekuwa taifa jipya duniani usiku wa kuamkia Jumamosi, lengo ambalo limefikiwa kufuatia mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mingi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wa Sudan Kusini wakisheherekea

Sudan lilikuwa taifa la kwanza kuitambua Rasmi Sudan Kusini.

Uhuru wa Sudan Kusini unafuatia mzozo kati ya Kusini na Kaskazini uliosababisha vifo vya watu milioni 1.5.

Sherehe za uhuru zilianza saa sita kamili saa za Sudan Kusini mjini Juba. Saa iliyowekwa katikati ya jiji ilipotimu saa sita kamili, wimbo mpya wa taifa ulipigwa kupitia televisheni ya taifa hilo.

Sudan Kusini inakuwa taifa la 193, na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, na pia kuwa taifa la 54 barani Afrika.