Corinthians inataka kumsajili Tevez

Klabu ya Manchester City imepokea ombi kutoka kwa klabu ya Corinthians inayoshiriki kwenye ligi kuu ya Brazil ya kutaka kumsajili nyota wake Carlos Tevez kwa kitita cha pauni milioni 35.

Image caption Carlos Tevez Mchezaji wa klabu ya Manchester City

Lakini pendekezo hilo huenda likakataliwa na wasimamizi wa Manchester City ambao hawataki kumuuza mchezaji huyo kwa kiasi cha fedha kama hicho.

Corinthians inatumahi kumsajili tena mchezaji huyo ambaye aliichezea klabu hiyo kuanzia mwaka wa 2004-2006.

Uamuzi huo umechukuliwa na klabu hiyo baada ya Tevez kutangaza kuwa anataka kukihama klabu ya Manchester City ili apate muda wa kuishi na familia yake.

Ripoti zinasema kuwa klabu ya Manchester City, imeonyesha dalili za kumuuza mchezaji huyo mradi ikiwa itapokea zaidi ya pauni milioni 40.

Tevez ni dhahabu kwetu-Manchester City

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kocha wa Manchester City akiinua kombe la FA

Corinthians itahitajika kuongeza fedha zaidi ili kuishawishi Manchester City, kumuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye aliongoza klabu hiyo kunyakuwa taji lao la kwanza kwa zaidi ya miaka 35, wakati waliposhinda kombe la FA mwezi Mei mwaka huu.

BBC imegundua kuwa Manchester City inajiandaa kumsajili mshambulizi wa Atletico Madrid, Sergio Aguero, pindi tu mkataba utakapoafikiwa kuhusu uuzaji wa Tevez.

Kocha wa Manchester City Roberto Mancini amehusishwa na mipango ya kutaka kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, lakini mipango hiyo itatekelezwa tu ikiwa Tevez atakihama klabu hiyo.