Joey Barton anyimwa visa ya Marekani

Kiungo wa Newcastle Joey Barton ameachwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachofanya ziara nchini Marekani kujinoa kwa Ligi Kuu ya England baada ya Ubalozi wa Marakani kumyima visa.

Image caption Joey Barton

Mwaka 2008 Barton alifungwa jela baada ya kukiri kumpiga mtu katikati ya mji wa Liverpool.

Mwaka huo huo alipewa adhabu ya kifungo cha nje kwa kumpiga mchezaji mwenzake wa Manchester City.

Barton, mwenye umri wa miaka 28, amesema anajuta kwa kutokuwemo katika msafara wa timu hiyo, lakini hatarajii kupewa upendeleo wowote zaidi ya mtu aliyefanya vitendo kama vyake.

Timu ya Newcastle inatazamiwa kuondoka siku ya Jumapili kuelekea Marekani, kwa ajili ya mechi dhidi ya Sporting Kansas, Orlando City na Columbus Crew.

Barton atasafiri kwenda Uholanzi akiwa na kikosi cha wachezaji wa akiba, kitakachocheza na Hollandia, FC Utrecht na Almere City.

Kiungo huyo alisema: "Kwa bahati mbaya, nimenyimwa visa kutokana na vitendo vyangu vya siku za nyuma."

"Kile ninachoweza kufanya ni kujirekebisha kama binadamu, kitu ambacho nimenuwia kukifanya."

Ameongeza: "Kwa mara nyingine, naomba radhi kwa mashabiki wote wa Newcastle nchini Marekani ambao nilitamani sana kukutana nao.

"Tutaonana siku zijazo."