Man City waikatalia Cornthians kwa Tevez

Manchester City imekataa dau la paundi milioni 35 kutoka klabu ya Corinthians ya Brazil inayotaka kumsajili mshambuliaji wao Carlos Tevez.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Carlos Tevez

Corinthians wana matumaini ya kumnasa mshambuliaji huyo hatari ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo msimu wa mwaka 2004-2006 na wanamtaka tena baada ya Tevez kueleza ana nia ya kuihama Manchester City kutokana na sababu za kifamilia.

Lakini Manchester City imekataa dau hilo la euro milioni 40 lililotolewa siku ya Jumanne.

City wanaonekana hawana haraka ya kufanya uamuzi wowote juu ya Tevez hadi kiasi cha pesa wanachohitaji kitakapofikiwa, wakiamini wao wameshikilia mpini kuamua wakati gani wataridhika kumuuza huku akiendelea kuwa mchezaji atakayeuzwa kwa kiasi kikubwa cha fedha na mkataba wake bado ni mrefu katika klabu hiyo.

Hata hivyo, usajili nchini Brazil utakamilika tarehe 20 mwezi wa Julai, kwa hiyo kuna muda mfupi sana wa kuweza kuzungumza na kukubaliana na Corinthians.

Mkataba wa Tevez inaaminika ni mshahara wa paundi 200,000 kwa wiki.

Tevez amekuwa akihusishwa na kuhamia vilabu vikubwa kadha vya Ulaya tangu alipotangaza nia yake ya kutaka kuondoka Manchester City, ikiwemo timu ya Inter Milan ya Italia, ambayo baadae ikajitoa katika mbio za kumchukua.