Mashirika kutoa misaada zaidi Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi wa kisomali huko Dadaab

Mashirika ya kutoa misaada kutoka Uingereza yamepanga kuingia kusini mwa Somalia kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa.

Kuwa muda mrefu juhudi za kuwasaidia watu nchini humo zimekuwa zikitatizika kutokana na hali mbaya ya usalama.

Mashirika ya kimataifa yaliwekewa marufuku kutekeleza majukumu yao katika maeneo yote ya Somalia chini ya uthibiti wa kundi la Al Shabaab linaloaminika kuwa na uhusiano na mtandao wa Al Qaeda.

Harakati hizo zimelenga kupunguza makali ya ukame katika ukanda wa Afrika mashariki ambapo watu milioni 10 wanakabiliwa na njaa.

wanachama wa kamati ya kimataifa inayoshughulika na majanga DEC wanajiandaa kuimarisha shughuli za kutoa misaada kusini mwa Somalia huku maelfu ya raia wakiendelea kukimbilia nchini Kenya na Ethiopia pamoja na mji wa Mogadishu.

Wiki iliopita kundi la Al Shabaab lilitangaza kuondoa marufuku iliowekea mashirika ya kigeni yanayotoa misaada na huduma za dharura nchini humo.

Serikali ya Marekani na Uingereza zimeorodhesha Al Shababa kama kundi la kigaidi.

Aidha baadhi ya nchi wafadhili zimeelezea hofu kwamba huenda chakula cha misaada kikaelekezwa kuwafaidi wapiganaji wa kundi hilo.