Mvulana apigwa risasi Tunisia

Haki miliki ya picha Afp
Image caption Maandamano Tunisia

Polisi wamesema, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 14 ameuliwa wakati wa maandamano kwenye mji wa Sidi Bouzid nchini Tunisia.

Aliuliwa kwa risasi kimakosa baada ya polisi kutawanya waandamanaji usiku, shirika la habari la Tap limeripoti.

Mkuu wa polisi Samir al-Meliti alisema majeshi ya usalama yalianza kufyatua risasi baada ya waandamanaji kurusha mabomu yenye petroli.

Kulikuwa na ripoti za maandamano katika maeneo mengine ya Tunisia siku ya Jumapili, ikiwemo Tunis.

Sidi Bouzid ndipo ambapo mapinduzi yalipoanza Desemba mwaka jana.

Mjasiriamali Mohammed Bouazizi alijiteketeza akipinga kunyanyaswa na maafisa wa eneo hilo.

Hatua hiyo ilisababisha maandamano ya kitaifa, yaliyosababisha kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu Zine al-Abidine Ben Ali kukimbia mwezi Januari.

Waandishi wanasema, miezi sita baadae, Watunisa wengi wanafadhaika kwa kukosekana maendeleo chini ya serikali mpya.

Polisi walirusha gesi za kutoa machozi kwa waandamanaji wakitaka mawaziri wajiuzulu kwenye mji mkuu, Tunis, siku ya Ijumaa .

Serikali imetupia lawama ghasia za hivi karibuni kwa waislamu wenye siasa kali.

Uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.