BAE yashutumiwa na Wabunge wa UK

Kampuni ya Uingereza inayotengeneza silaha na ndege za kijeshi, BAE Systems imeshutumiwa vikali na tume iliyoundwa na Bunge la Uingereza kuchunguza kesi ya rushwa kuhusu Radar ambayo shirika hilo liliiuzia Tanzania.

Image caption BAE isipolipa itakiona

Wabunge wameituhumu BAE kwa mpango wake wa malipo kwa Tanzania na kuutaja kama ''unafiki mtupu''.

BAE imekiri kuwa haina kumbukumbu ya maandishi kuhusu malipo ya pauni milioni 8 sawa na dola milioni 12 za Marekani kwa wakala aliyesimamia biashara hiyo.

Hata hivyo, baada ya kujitetea, kampuni haikupatikana na hatia nyingine zaidi kuwa ilishiriki rushwa.

Mvutano huu unahusu Radar ya kuongoza safari za ndege iliyouziwa Tanzania mwaka 1999.

Hata hivyo hili huenda kikawa kigezo kwa wakereketwa wanaopinga rushwa wanaodai kuwa hongo na rushwa ni kizuizi cha maendeleo ya uchumi.

Katika kujitetea mbele ya mamlaka yaliyoendesha kesi hiyo, afisi inayosikiliza kesi za ufisadi wa kupindukia(Serious Fraud Office) BAE imekubali kuwalipa raia wa Tanzania pauni milioni 30.

Haki miliki ya picha tanzania parliament
Image caption Kikao cha Bunge Tanzania

Kiwango cha pauni hizo milioni 30 ni fidia kwa Tanzania kwa sababu ya kufedheheshwa kwa malipo ya pauni milioni 8 pamoja na madai ya kuwauzia Tanzania mtambo wa matumizi ya kijeshi wasiouhitaji na kwa gharama kubwa.

Hata hivyo Shirika la BAE pamoja na mamlaka ya kuchunguza ufisadi hayakuweza kusema kama pesa hizo milioni 8 zilitumiwa kama hongo ya kuficha mauzo ya radar hiyo.

Wakili mkuu wa BAE, Philip Bramwell, alisema kuwa kampuni hiyo imesikitishwa na matukio yote na kuomba radhi. Wakili huyo alikiri kuwa kampuni hiyo kamwe haitorudia kutoa malipo ya aina hiyo.

Wabunge wa Kamati nyingine ya Maendeleo ya Kimataifa wamepuuza msimamo wa kampuni hiyo na kuutaja kama usioridhisha.

Walirudia matamshi ya Jaji mmoja aliyesema kuwa mradi mzima ulikuwa ni aibu tupu, na ukitizama malipo ya pauni milioni 8 lazima ushuku na kuna uwezekano mkubwa kuwa kitita hicho kilitumiwa wakati wa majadiliano ya kutaka kampuni ya BAE ipendelewe katika kuuza radar hiyo.

Wabunge hao wakauliza kwanini hadi wakati huu kampuni hiyo imeshindwa kulipa angalau sehemu ya pauni hizo milioni 30.

Vilevile walihoji jinsi gani kampuni hiyo ilivyoweza kuunda bodi yake binafsi iliyofikia uwamuzi wa jinsi fedha hizo zingetumiwa badala ya kuzikabidhi moja kwa moja kwa serikali ya Tanzania, kama lilivyotaka kundi la wabunge kutoka Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Malcolm Bruce MP akauliza kama si dharau na matusi kwa kampuni hiyo kutoa mapendekezo ya namna pesa hizo zitakavyotumiwa na kujifanya kuwa inaelewa zaidi kuliko serikali ya Tanzania jinsi ya kutumia pesa zake.

Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka inayochunguza rushwa, Richard Alderman, aliyekuepo mbele ya Kamati hiyo alisema kuwa ameshangazwa kuona kuwa malipo hayo yamechelewa.

Alijitolea kuiandikia BAE kuuliza sababu za kuchelewa na kuongezea kuwa wakizidi kuchelewesha malipo hayo huenda wakakabiliwa na adhabu nyingine.