Kanali wa Colombia ahukumiwa kuwaua raia

Kanali wa jeshi la Colombia amehukumiwa kifungo cha miaka 21 gerezani, huku hukumu hii ikiwa imepunguzwa kutoka kifungo cha miaka 42 baada ya kukiri kuwa Kikosi chake kimewaua raia wapatao 57 ambao waliwavisha sare za waasi na kudai kuwa walikuwa waasi wanaofuata siasa za Ki-maxi.

Kanali Luis Fernando Borja, amekiri kuhusika na mauaji ya watu wawili mwaka 2007, ambapo mauaji hayo yalitekelezwa kwa ushawishi wa ahadi za ajira, kwa kuwavisha watu hao sare na kudai walikuwa ni waasi wa Ki-maxi wakiwa wamevaa mavazi yao ya mapambano.

Pia alikiri kulikuwa na raia wengine 55 waliouliwa na kikosi chake katika mazingira sawa na hayo. Hii ni mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu kupatikana na hatia ya kashfa ya kuhadaa, kinyume na isivyotakiwa kufanywa.

Ofisi ya mwanasheria mkuu inachunguza zaidi ya matukio 1400 yanayohusu maelfu ya watu walioathirika na ukatili kama huo. Kashfa hiyo inadhaniwa ilichangiwa na tamaa kutokana na sehemu ya utamaduni wa jeshi wa tuzo, ambapo wanajeshi walikuwa wakituzwa kutokana na kuwauwa waasi.

Sehemu kubwa ya hadaa hiyo ya jeshi ilitokea chini ya uongozi wa vipindi viwili wa Rais Alvaro Uribe. Anasifika kwa kukukabiliana na waasi wa Ki-maxi waliokuwa wakitishia kuangusha utawala wake, lakini kwa sasa swali lililopo ni kwa gharama ya kiasi gani mafanikio yalipatikana ikitiliwa maanani kukiukwa kwa haki za binadamu.