Mzozano katika serikali ya Kenya

Wakimbizi kutoka Somalia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi kutoka Somalia

Serikali ya Kenya inakabiliwa na mzozo wa ndani kwa ndani kuhusu kuongezeka kwa Wasomali wanaokimbilia nchi hiyo kutokana na ukame mbaya kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 60.

Wasomali wapatao 370,000 wamesongamana katika kambi moja na serikali ya Kenya imejikuta kugawanyika kuhusu suala la kufungua kambi ya pili.

Waziri mmoja amesema kambi mpya itawapa moyo Wasomali zaidi kuvuka mpaka na kuingia Kenya.

Waziri mwengine nae amesema inaabisha kuwa serikali ya Kenya inakataa kuwapa msaada zaidi wakimbizi.

Siku ya Jumatatu mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi Antonio Guterres alifanya mazungumzo na Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya George Saitoti kuomba kambi ya Ifo II ifunguliwe.

Kambi hiyo inaweza kuwahifadhi watu 40,000 na itasaidia kupunguza msongamano katika kambi ya Dadaab iliyoko karibu na mpaka wa Somalia.

Wafanyikazi wa misaada katika kambi ya Dadaab wanasema kuwa hali katika kambi hiyo ni mbaya sana kutokana na msongamano wa watu 370,000 katika eneo lililokusudiwa watu 90,000.

Siku ya Jumatano, naibu Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya Orwah Ojodeh aliiambia BBC kuwa kambi mpya haitokuwa suluhisho la matatizo ya njaa yaliopo sasa.

Bw Ojodeh aliongeza kusema kuwa msaada wa chakula ndio unafaa utolewe nchini Somalia kwa kuwa njaa na wala sio ukosefu wa usalama ndio sababu kuu ya Wasomali wengi kukimbilia nchini Kenya.

Lakini Waziri wa Uhamiaji Otieno Kajwang amesema anaona aibu kuwa serikali ya Kenya inakataa kufungua kambi ya Ifo II. Bw Kajwang amesema hili linatokea wakati Umoja wa Mataifa tayari umeshaipa Kenya maelfu ya dollar kwa ajali ya Kambi hiyo.

Bw Kajwang amewalaumu wakuu wa usalama na maafisa wengine katika afisi ya rais akisema ndio wanaosababisha kambi hiyo isifunguliwe.

Mwandishi wetu wa BBC Will Ross anasema shirika la chakula duniani WFP linatathmini uwezekano wa kuongeza shughuli zake nchini Somalia.

Hatahivyo WFP inasema haitaweza kurejea katika maeneo yanayosimamiwa na wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabab hadi litakapopewa hakikisho la usalama wake.

Wiki jana al-Shabab ilisema imeondoa marufuku iliyoweka dhidi ya mashirika ya kigeni ya misaada ikiwa hayatakuwa na azma nyengine mbovu.